WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Prof. Riziki Silas Shemdoe (Mb), ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kazi kubwa ya kuunganisha mawasiliano ya barabara kutoka kijiji hadi kijiji na wilaya hadi wilaya, akisema kuwa jukumu hilo ni gumu na linahitaji weledi, uzalendo na utendaji wa hali ya juu.

Prof. Shemdoe alitoa pongezi hizo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Isago lenye urefu wa mita 42.6 katika Kata ya Mngeta, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, mkoani Morogoro, akiwa katika ziara ya kikazi ya tarehe 2 hadi 6 Julai 2026 Mkoani humo.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya mradi iliyosomwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, Waziri Shemdoe amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara na madaraja ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

"TARURA mmefanya kazi kubwa sana ya kuunganisha wananchi kupitia mtandao wa barabara vijijini. Kazi hii si rahisi; inahitaji utaalamu, kujituma na uwezo wa kufanya kazi katika mazingira magumu. Serikali inatambua mchango wenu na inawapongeza kwa juhudi zenu za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri na usafirishaji wakati wote," amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, Waziri huyo aliwataka mkandarasi na mshauri wa mradi kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha za umma na ubora wa kazi zinazotekelezwa.

Mhandisi Emmanuel Ndyamukama ni Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, amesema mradi wa ujenzi wa Daraja la Isago ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuboresha miundombinu katika maeneo ya uzalishaji vijijini, kuimarisha uchumi na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na majanga ya asili.

Mkataba wa ujenzi wa daraja hilo ulisainiwa tarehe 15 Desemba 2025 kati ya Katibu Mkuu wa TAMISEMI na kampuni ya ENGISOFT Company Limited kwa thamani ya shilingi bilioni 1.738 (bila kodi), huku usimamizi wa mradi ukifanywa na kampuni za LUPTAN Consults Ltd kwa kushirikiana na Afro Base & ORU Consults.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 42.6, barabara za maingilio zenye urefu wa mita 300, ujenzi wa makalvati mawili pamoja na kuinua tuta katika eneo la mradi.

Utekelezaji ulianza rasmi Januari 1, 2026 na unatarajiwa kukamilika Agosti 30, 2026. Hadi sasa, utekelezaji umefikia asilimia 20, huku mkandarasi akiwa amelipwa malipo ya awali yenye jumla ya shilingi milioni 260.7.

Daraja la Isago linatarajiwa kuunganisha kwa urahisi maeneo ya kilimo kati ya Mngeta na Isago, kurahisisha usafiri wa wananchi kufikia huduma muhimu za elimu, afya na biashara, pamoja na kupunguza athari za mafuriko ambazo zimekuwa zikisababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Mhandisi Ndyamukama imesema mradi umekumbwa na changamoto ya kuchelewa kwa utekelezaji kutokana na mvua kubwa za msimu zilizonyesha mkoani Morogoro na kuathiri baadhi ya shughuli za ujenzi.

Kwa upande wao Watumiaji wa Barabara na wakazi wa Kata ya Mngeta akiwemo Rajabu Sudi amesema kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kwenda sokoni, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji katika eneo hilo.

Nae Elizabeth Sanga mkazi wa Kijiji cha Isago amesema kwa miaka mingi walikuwa wakipata shida kuvuka eneo hilo kipindi cha mafuriko, hali iliyosababisha wanafunzi kukosa masomo, wagonjwa kushindwa kufika kwenye vituo vya afya kwa wakati na wafanyabiashara kuchelewa kufikisha bidhaa zao sokoni.

Amesema ujenzi wa daraja hilo ni suluhisho la kudumu ambalo litabadilisha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

NA FARIDA MANGUBE