Aliyekuwa waziri wa Zambia amesemekana aliuawa katika uvamizi uliofanywa na vikosi vya usalama katika nyumba inayosemekana kuwa ya kiongozi wa upinzani Brian Mundubile, siku moja baada ya uchaguzi wa urais Zambia.

Msemaji wa polisi amesema Mutotwe Kafwaya alijeruhiwa vibaya na kufariki baada ya kupigwa risasi na maafisa wa usalama wakati wa kile ambacho mamlaka zimesema kilikuwa ni majibizano ya risasi katika operesheni ya kiusalama mjini Lusaka siku ya Ijumaa.

Watu 11 walikamatwa katika uvamizi huo, huku mamlaka zikiishutumu chama cha NRPUP, kinachoongozwa na Mundubile, kwa “kuhusika na uasi” na “shughuli za kijeshi za wanamgambo”, pamoja na kuhifadhi silaha za “kiwango cha juu”.

Mundubile, ambaye tangu wakati huo amejificha, ameyapinga madai hayo na kuyaita “uzushi.”

Kulingana matokeo rasmi, Rais aliye madarakani Hakainde Hichilema alishinda muhula wake wa pili wa miaka mitano kwa kupata asilimia 60 ya kura. Mundubile, alishikilia nafasi ya pili kwa asilimia 38, na amepanga kupinga matokeo hayo mahakamani baada ya kudai kuwa mchakato wa kujumlisha kura uliingiliwa.

Polisi walithibitisha kifo cha Kafwaya Jumatano usiku, huku kukiwa na ongezeko la madai ya kutaka mamlaka kutoa taarifa kuhusu kilichotokea.