
GEITA; KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP), Safia Jongo amezitaka halmashauri kuandaa mpango wa mapema kudhibiti ongezeko na uendeshaji holela wa bajaji na pikipiki katikati ya mji.
Kamanda Jongo ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika ofisi ya mkuu wa mkoa, huku akiitaja Manispaa ya Geita kama waathirika wakubwa wa ongezeko la bajaji na pikipiki.
Amesema Mji wa Geita ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi, lakini kumekuwa na wimbi kubwa la bodaboda na bajaji za abiria, hali inayosababisha foleni na misongamano isiyo ya lazima na kuhatarisha usalama wa barabarani.
“Kutokana na changamoto za mji kukua na watu kuwa wengi, sasa barabara ni ndogo halmashauri ya manispaa iweke mkakati wa kupunguza bajaji na pikipiki mjini.
“Kwa sababu imekuwa ni changamoto, wanaovateki, barabara ni ndogo lakini kuna msongamano mkubwa wa bajaji na pikipiki ukilinganisha na ufinyu wa barabara,” amesema.
Kamanda Jongo amesema mkakati wa haraka unapaswa kuandaliwa kuzifanya bajaji zitoe huduma nje ya mji na kuiacha barabara kuu iweze kuhudumiwa na mabasi madogo ya abiria maarufu kama daladala.
Pia amesema kuna changamoto kubwa ya vituo holela vya kupakia na kushusha abiria kwa mabasi ya abiria, jambo linalohitaji udhibiti wa haraka ili kupunguza wimbi la ajali.
“Kuna changamoto ya vituo holela vya kushusha na kupakia abiria kwa mabasi madogo na makubwa kwenye maeneo yasiyo rasmi wanasababisha msongamano na hatimaye ajali.
“Ni vyema tufanye upembuzi yakinifu upya, tuweke vituo vya muda, Mwatulole na Magogo kwa sababu mji umesogea na watu wanaona mbali kutoka kule kuja mjini kufuata vituo vya mabasi,” amesema SACP Jongo.
Mwenyekiti wa Waendesha Bajaji mkoani Geita, Mussa Kisoke amesema mpaka sasa Manispaa ya Geita ina jumla ya bajaji 1,680, Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro bajaji 321 na Chato bajaji 210.
Ameongeza pia njia panda ya Mganza kuna bajaji 50, eneo la Bwanga bajaji 65, mji mdogo wa Runzewe bajaji 154, wilaya ya Nyang’hwale bajaji sita huku bajaji nne katika Kata ya Nzera.
Mwenyekiti wa Madereva wa Bodaboda Mkoa wa Geita, Fred Fidelis amesema mpaka sasa kuna takribani wanachama 5,000 wanaotambuliwa katika kata 13 za Manispaa ya Geita.
Fred amesema pia jumla ya maegesho rasmi 123 yanayotambuliwa yamesajiliwa ndani ya Manispaa ya Geita, ambapo bodaboda wote wamepewa vitambulisho kwa ajili ya utambuzi.
0 Comments