
DAR ES SALAAM; Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa kampeni maalumu ijulikanayo kama ‘AFCON Kitaa 2027’, ambayo itazinduliwa rasmi Oktoba 30, 2026 jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TASWA, Amir Mhando, imesema kampeni hiyo ni mahususi kwa wanataaluma ya habari kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika nchini mwaka 2027 na itahusisha matukio ambayo TASWA itayafanya kuelekea fainali hizo, ambazo Tanzania itaandaa kwa ubia na nchi za Kenya na Uganda.
Amesema Kampeni ya AFCON Kitaa 2027 inatarajia kufikia makundi mbalimbali kuanzia wanahabari, wanamichezo, wanasiasa, wafanyabiashara, watumishi wa umma, wajasiriamali, vijana, wanawake na wanafunzi kuyataja kwa uchache, lengo Watanzania wote tuimbe wimbo mmoja kwamba AFCON 2027 ni fursa ya kitaifa.
“Pia kuelekea uzinduzi rasmi wa AFCON Kitaa 2027, TASWA itaendesha warsha na makundi ya wanahabari kwa awamu tofauti, ikiwa ni mwendelezo wa mpango wake iliouanzisha Aprili, 2026 jijini Dar es Salaam ujulikanao kama Mustakabali wa Uandishi wa Habari za Michezo ‘The Future Of Sports Journalism’.

“Makundi hayo ni waandishi wa habari chipukizi, waandishi wa habari waandamizi, wachambuzi wa habari za michezo, wahariri wa habari za michezo. Pia itakutana na viongozi wa michezo wa sasa na wa zamani, lengo ikiwa ni kutazama mwelekeo wa uandishi wa habari za michezo na pia ujio wa AFCON Kitaa 2027,” amesema.
Amesema Aprili 24, 2026 TASWA ilianza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Mustakabali wa Uandishi wa Habari za Michezo kwa kuendesha warsha iliyohusisha wanahabari chipukizi, wahariri wa habari za michezo na waaandishi magwiji wa habari za michezo, ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo masuala ya rushwa kwenye michezo iliyotolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
0 Comments