Uganda na Tanzania zimezindua ushirikiano mpya wa nishati unaolenga kuifanya bandari ya Tanga kuwa kitovu muhimu cha nishati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mpango huo unatarajiwa kuvutia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 20, huku ukiwa na mpango wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta pamoja na miundombinu mingine ya nishati.
Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta Uganda, UNOC, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC, pamoja na kampuni ya Vitol Bahrain EC.
Mpango huo utaweka msingi wa ushoroba jumuishi wa nishati itakayounganisha Uganda na Tanzania kupitia mabomba ya kusafirisha bidhaa mbalimbali za mafuta, pamoja na miundombinu ya mafuta na gesi na vituo vya kuhifadhi nishati.
Uganda na Tanzania zinasema ushirikiano huo unaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya mafuta na nishati katika Afrika Mashariki, huku Bandari ya Tanga ikitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mnyororo huo wa nishati.
Haya yanajiri baada ya tajiri mkubwa barani Afrika Aliko Dangote kuchagua bandari ya lamu kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta, badala ya Tanzania kama ilivyokuwa imependekezwa.
0 Comments