Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.


Waziri Mkuu amefanya ziara hiyo leo Jumapili, Agosti 23, 2026, ambapo baada ya kuwasili hospitalini hapo ametembelea wodi mbalimbali, zikiwemo Wodi ya Mama na Mtoto pamoja na Wodi ya Upasuaji.

Akiwa katika wodi hizo, Dkt. Nchemba amezungumza na wagonjwa pamoja na ndugu zao, kusikiliza maoni yao kuhusu huduma wanazopata na kufahamu changamoto zinazowakabili wakati wa kupata matibabu.

Wananchi waliokutana na Waziri Mkuu wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Serikali kwa juhudi zinazoendelea katika kuboresha huduma za afya na mazingira ya utoaji wa huduma hospitalini.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia kwa karibu utoaji wa huduma za kijamii na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa wakati na katika mazingira yanayokidhi mahitaji yao.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; pamoja na viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala.