Takriban watu 20 wameuawa, wakiwemo watoto, na wengine kadhaa hawajulikani walipo baada ya jengo lililoharibiwa na vita kuporomoka katika Ukanda wa Gaza, kulingana na timu za uokoaji za eneo hilo.
Picha za video zinaonyesha shughuli za kutafuta miili na manusura zikiendelea kwenye vifusi vya jengo hilo la ghorofa nyingi katika eneo la Tal al-Hawa jijini Gaza, ambapo sakafu zake zilikuwa zimebonyeana na kuangukiana.
Wakazi walisema familia 10 zilikuwa zikiishi katika vyumba hivyo licha ya maonyo kwamba jengo hilo halikuwa salama.
Wafanyakazi wa huduma ya uokoaji ya Ulinzi wa Raia inayoendeshwa na Hamas walisema kuwa mwanzoni walikuwa wakifanya kazi "bila zana zozote" kutokana na vikwazo vikali vya Israel dhidi ya vifaa vinavyoruhusiwa kuingizwa Gaza.
Hata hivyo, baadaye waliweza kukopa mitambo mizito.
Siku ya Jumanne, mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza yaliua angalau Wapalestina watano, wakiwemo watoto wawili na kamanda wa Hamas, kulingana na maafisa wa afya na vyanzo vya Hamas.
Jeshi la Israel lilisema liliua kamanda wa Hamas kusini mwa Gaza na mpiganaji mwingine kaskazini. Katika matukio yote mawili, mtoto mmoja pia aliripotiwa kuuawa.
Kando na hayo, shirika la hisani la Uingereza la Medical Aid for Palestinians lilisema kuwa mgonjwa mmoja aliuawa na ndege isiyo na rubani ya Israel katika kituo cha afya kinachosaidiwa na shirika hilo huko Jabalia, kaskazini mwa Gaza.
0 Comments