
KIGOMA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma kimezitaka halmashauri za mkoa huo kushughulikia changamoto zinazokwamisha miradi ya maendeleo ili iweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi licha ya kukamilika kwa baadhi ya majengo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Jamal Tamim, wakati akiongoza Kamati ya Siasa ya chama hicho kukagua miradi ya maendeleo wilayani Buhigwe na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Akiwa katika Kituo cha Afya Rusaba wilayani Buhigwe, Tamim alishuhudia kituo hicho kushindwa kuanza kutoa huduma za upasuaji kutokana na ukosefu wa huduma ya maji, licha ya majengo ya huduma hiyo kukamilika.
Aidha, kamati hiyo ilibaini kuwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Bilate, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, kimeshindwa kuanza kutoa huduma licha ya kukamilika miaka miwili iliyopita, kwa sababu ya kuhitaji kupakwa rangi upya baada ya rangi ya awali kuchakaa.
Tamim alisema hali hiyo haikubaliki, akieleza kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, hivyo ni jambo lisilofaa miradi kushindwa kutoa huduma kwa sababu ya changamoto zinazoweza kutatuliwa.
Alizitaka halmashauri kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa wakati na kuwataka wakuu wa wilaya kuwa wakali katika usimamizi wa miradi ili kuhakikisha inakamilika na kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Afya Rusaba, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Yohana Milinde, alisema jumla ya majengo tisa yamejengwa katika mradi huo ambao umegharimu Sh milioni 770.
Milinde alisema kuwa baada ya kukamilika kwa majengo ya kipaumbele, ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje, jengo la huduma za uzazi na jengo la upasuaji, baadhi ya huduma zilianza kutolewa.

Hata hivyo, alisema huduma za upasuaji hazijaanza kutokana na kutokuwepo kwa huduma ya maji, huku jitihada zikiendelea kufanyika kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa ili huduma hizo zianze kutolewa kwa wananchi.
0 Comments