.

Shirika la utangazaji la Marekani, CNN, limezuiwa kusafiri pamoja na Rais Donald Trump ndani ya ndege ya rais ya Air Force One wakati wa safari yake kuelekea jimbo la Tennessee siku ya Jumamosi.

Hatua hiyo ni ya hivi karibuni katika mvutano unaoendelea kati ya Ikulu ya Marekani na vyombo vya habari, baada ya White House kulazimika kuondoa marufuku iliyokuwa imeweka dhidi ya baadhi ya taasisi za habari.

CNN ilikuwa imepangwa kuandamana na Trump katika safari yake ya Tennessee kuhudhuria mechi ya mpira wa miguu wa vyuo vikuu nchini Marekani. Hata hivyo, ratiba ya vyombo vya habari iliyotolewa na White House usiku wa Ijumaa haikuonyesha jina la CNN.

BBC imeiomba White House kutoa maoni kuhusu uamuzi huo.

CNN imeripoti kuwa hakuna chombo kingine cha habari kilichotajwa kuchukua nafasi yake katika ratiba ya muda ya rais.

Wiki iliyopita, Trump aliwapiga marufuku waandishi wa habari wa CNN, Politico na MS NOW kuingia White House, akiwatuhumu kuchapisha "taarifa za kubuni au uongo" kuhusu utawala wake.

Vyombo hivyo vitatu vya habari vilisema vinachukua hatua za kisheria dhidi ya uamuzi huo na kumtuhumu Trump kwa kukiuka haki zao za kikatiba za uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Wakati huo huo, mitandao minne ya televisheni ambayo hushiriki kwa zamu kuripoti shughuli za White House pamoja na CNN, yaani ABC, CBS, Fox News na NBC, ilisimamisha kwa muda matangazo ya shughuli za rais kama ishara ya mshikamano na vyombo vilivyowekewa marufuku.