DODOMA: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amewataka wanawake kutafuta elimu na kujiimarisha kiuchumi, ili waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika familia na malezi ya watoto.

‎Dk Gwajima amesema wanawake wanapaswa kuweka mkazo katika kupata elimu na kujenga uwezo wa kiuchumi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kukabiliana na changamoto za maisha.



Amesema hayo leo Septemba 23, 2026, jijini Dodoma, wakati wa Mkutano wa Nusu Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.

Mkutano huo umefanyika ukiwa na kaulimbiu ‘Malezi Bora kwa Watoto: Msingi wa Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050’.



‎“Wamama mnakwama wapi? Wamama tutafute elimu kwanza, wamama tutafute kuimarisha kiuchumi kwanza,” amesema Dk Gwajima.

‎Amesema baadhi ya wanaume na wanawake hukutana mtaani, kuanzisha mahusiano na kupata watoto bila kuwapelekea wazazi wao au kufuata taratibu za kifamilia na kuongeza kuwa wanaposhindwana katika mahusiano, baadhi ya wanawake huachwa na changamoto za malezi ya watoto, huku wazazi hao kushindwa kutatua changamoto zinazowakabili watoto.

‎Ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia umuhimu wa wanawake kujenga uwezo wao, ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika familia na malezi ya watoto.