WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameipongeza Serikali ya Qatar kwa kufanikiwa kuwa na matumizi makubwa ya teknolojia kwenye usafiri wa umma na hasa matumizi ya nishati safi.
Ametoa pongezi hizo leo (Jumamosi, Septemba 26, 2026) jijini Doha, Qatar mara baada ya kupokea taarifa ya uendeshaji wa kampuni ya usafirishaji ya MOWASALAT kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdullah bin Mohammed Al Thani.
Waziri Mkuu ambaye ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini humo, amesema ubunifu wao umesaidia kuondoa msongamano wa magari barabarani kwa sababu usafiri wa umma ni wa uhakika.
"Nyumbani tunalo tatizo la msongamano wa magari na kupitia teknolojia mnazotumia, Tanzania inaweza kujifunza mbinu mlizotumia ili nasi tuweze kukabiliana nalo," amesema.
Waziri amesema amefurahi kuona kampuni yao inatumia nishati safi kwa sehemu kubwa. "Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa nishati safi barani Afrika, na hii ni hatua nzuri kwetu. Tunatarajia kuwa wenyeji wa AFCON 2027, kwa hiyo itatufaa sana," amesema.
Waziri Mkuu ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwaajiri Watanzania 722 katika nafasi mbalimbali. "Ni fursa kwa vijana wetu kukuza ujuzi na kujifunza teknolojia mbalimbali."
Mapema, Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdullah bin Mohammed Al Thani alimweleza Dkt. Mwigulu kwamba kampuni hiyo inatoa huduma za usafiri wa abiria kwa kutumia mabasi, taxi, usafiri kwa wanafunzi, matukio binafsi, ya kitaifa na ya kimataifa.
"Kwa mwaka 2025, kampuni yetu imetoa huduma kwa watu milioni 42. Tunayo magari 1,200 na njia za magari (routes) tulizonazo ni 128. Asilimia 70 ya magari yetu yanatumia umeme na kutokana na ubora na uhakika wa huduma zetu, tumeweza kuyatoa barabarani magari 12,363," alisema.
Alisema kutokana na teknolojia walizonazo, magari yao yanakuwa yanakaguliwa kwa mfumo wa kielektroniki. Yamewekewa mfumo unaowezesha kubaini changamoto kwa haraka badala ya kusubiri kufanyiwa ukaguzi na mafundi," alisema.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


0 Comments