Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu amesema kuwa miongoni mwa masuala ambayo kamati hiyo itahakikisha inatekeleza ni pamoja na kufanikisha kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi Tanzania (Tanzania Geoscientists’ Registration Board).
Mgalu amesema hayo Jumatatu Septemba 14, 2026 Jijini Mwanza wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wajiolojia Tanzania ambapo alishiriki kama mgeni rasmi katika tukio hilo akiambatana na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mgalu amesema kuwa kukosekana kwa bodi ya kusimamia weledi wa kada ya wanajiosayansi kumesababisha uwepo wa vishoka wanaofanya kazi za kijiolojia bila ya kuwa na sifa stahiki hivyo kusababisha hasara kwa wawekezaji na Serikali kwa ujumla.
“Jambo hili limesababisha kutokukuwepo kwa mfumo thabiti wa kudhibiti maadili, viwango, taaluma, weledi na utaalamu wa wanajiosayansi walio katika utumishi wa umma na katika sekta binafsi nchini”
Kwa upande wao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walioshiriki Mkutano wa Wajiolojia kwa mwaka 2026 akiwemo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma na Mbunge wa Jimbo la Katoro, Kija Ntemi wamesema suala la uanzishwaji wa Bodi ni la msingi watahakikisha wanaibeba ajenda hii kikamilifu.

0 Comments