Faith Kipyegon raia wa Kenya ameshinda mataji matano katika mashindano ya dunia na medali tatu za dhahabu za Olimpiki.

Jiji la Nairobi Kenya, limeshinda uenyeji wa mashindano maarufu ya riadha ya dunia ya mwaka 2029 baada ya kuibwaga miji ya London (Uingereza) na Roma (Italia).

Kwa hatua hiyo Kenya itakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa mashindano hayo ya riadha ya dunia.

Rais wa shirikisho la riadha duniani Sebastian Coe, alielezea ushindi huo kwa Nairobi ni wenye mvuto na mguso mkubwa.

Umahiri wa Kenya kwenye riadha kimataifa umekuwa moja ya sababu kubwa zilizochangia Kenya kushinda nafasi hiyo.

Nchi hiyo imetoa mabingwa wengi wa Olimpiki na dunia; miongoni mwao ni Eliud Kipchoge, mshindi wa mbio za marathon katika Olimpiki mara mbili, ambaye alishiriki katika kuwasilisha hoja za kuunga mkono Nairobi wakati wa mchakato huu.

Uamuzi huu ni wa kihistoria, kutokana na hoja kwamba Afrika haijawahi kuandaa mashindano ya dunia ya riadha ya ngazi ya juu, licha ya kuzalisha baadhi ya nyota wakubwa zaidi wa mchezo huo.

Kenya ilisisitiza uzoefu wake katika kuandaa hafla nyingine kubwa katika muongo uliopita, ikiwemo mashindano ya dunia ya riadha ya nje ya Uwanja (World Cross Country Championships) mjini Mombasa, pamoja na Mashindano ya dunia ya Vijana (chini ya umri wa miaka 18 na 20) jijini Nairobi.

Awali, mji mkuu wa Kenya Nairobi iliomba kuandaa mashindano ya dunia ya mwaka 2025 lakini ikashindwa na Tokyo, huku udhaifu mkubwa ukiwa ni suala la miundombinu.

Safari hii, nchi hiyo ilionyesha maboresho yaliyofanywa kwenye viwanja na vifaa vilivyopo kama ushahidi wa utayari wake, huku viwanja vikifanyiwa ukarabati kujiandaa kwa ajili ya michuano ya soka ya kombe la mataifa ya Afrika mwakani.

Wakati huo huo, jiji la Munich lilipata haki ya kuandaa mashindano ya dunia ya riadha ya mwaka 2031.