Rais William Ruto amewaonya watu anaowatuhumu kujaribu kuvuruga ujenzi wa kiwanda cha kusafishia mafuta cha Dangote huko Lamu, mradi unaokadiriwa kugharimu Sh2.2 trilioni.
Akizungumza Kilifi Jumanne wakati wa hafla ya utoaji wa hati miliki, Ruto amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kubadilisha uchumi wa Kenya na kuvutia uwekezaji mkubwa wa kigeni.
“Kesho, Mungu akipenda, tutafanya rasmi uzinduzi wa kiwanda cha kusafishia mafuta cha Lamu,” alisema Ruto.
Ruto amewaonya wanaopinga uwekezaji huo dhidi ya kujaribu kuvuruga mradi huo kwa kuweka masharti mbalimbali, ikiwemo kudai hisa katika kiwanda hicho.
“Safari hii hamtafanikiwa kutudanganya wala kutupotosha,” alisema Rais Ruto.
Ruto pia aliwashutumu watu aliowaita “madalali” kwa kuchangia kupotea kwa baadhi ya uwekezaji mkubwa nchini Kenya hapo awali. Alitoa mfano wa jaribio la awali la Dangote kujenga kiwanda cha saruji nchini Kenya, pamoja na uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta ghafi la Uganda kupitia Tanzania badala ya Kenya.
Rais anatarajiwa kuongoza hafla ya uzinduzi wa mradi huo Lamu Jumatano.
Kiwanda hicho, kinachoungwa mkono na mfanyabiashara wa Nigeria Aliko Dangote, kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku.
0 Comments