Marekani imethibitisha kuwa imetuma silaha ya angani katika obiti ya Dunia, ikiwa ni mara ya kwanza kukiri kuwa na uwezo kama huo wa mashambulizi.

Waziri wa Jeshi la Anga la Marekani, Troy Meink, amesema silaha hiyo iliyopo kwenye obiti ilikuwa muhimu ili kulinda vikosi vya Marekani dhidi ya vitendo vya uhasama vya adui.

Akizungumza katika Kongamano la Anga, Nafasi ya Anga na Mtandao (Air, Space and Cyber​​Conference) siku ya Jumatatu, Meink alisema Marekani iko tayari kukabiliana na "vitisho vinavyobadilika", lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu uwezo wa silaha hiyo au wakati ilipowekwa kwenye obiti.

Viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi hapo awali walisema walipanga kuimarisha uwezo wa kijeshi angani, wakitaja mipango ya Urusi na China ya kutengeneza njia za kushambulia na kuvuruga satelaiti za Marekani katika mzozo wa siku zijazo.

Utawala wa Trump umesema kuwa uwezo wa kijeshi wa angani - na makombora ya kuzuia mashambulizi - ni sehemu muhimu ya mfumo wake wa ulinzi unaopangwa kuitwa "Golden Dome" ili kuilinda Marekani dhidi ya makombora na vitisho vingine vya angani.

Mkataba wa mwaka 1967 ulipiga marufuku silaha za maangamizi makubwa katika obiti. Tangu wakati huo, mataifa yenye nguvu kubwa ikiwemo Marekani, Urusi, na China yamekuwa yakichunguza uwezo mwingine nje ya mkataba huo, kama vile kulenga satelaiti za wapinzani - ambazo ni muhimu kwa mawasiliano ya kijeshi, ufuatiliaji na urambazaji.

Mwaka jana, Rais Donald Trump alitoa agizo la kiutendaji likisisitiza jukumu la Jeshi la Anga la Marekani (US Space Force) si tu katika kulinda rasilimali, bali pia kama nguvu ya kushambulia.

Jeshi la Anga la Marekani - tawi jipya zaidi la jeshi la Marekani katika kipindi cha zaidi ya miaka 70 - lilianzishwa mwaka 2019 kama njia ya kulinda rasilimali za Marekani angani, ikiwa ni pamoja na mamia ya satelaiti zinazotumiwa kwa mawasiliano na ufuatiliaji.