Mfalme Charles amewaonya viongozi wa kampuni za akili mnemba kuhusu "hatari za kuwepo" zinazoweza kusababishwa na teknolojia hiyo ikiwa itaangukia mikononi mwa watu wasiofaa.
Alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kilele aliouitisha katika Dumfries House, Scotland, kujadili namna teknolojia hiyo inavyoweza kutumika kunufaisha jamii.
Waliohudhuria mkutano huo pia walijumuisha Kanishka Narayan, Waziri wa AI wa Uingereza, mshauri wa Papa, pamoja na wawakilishi kutoka kampuni kubwa za AI kama Nvidia, OpenAI na Anthropic.
Mkutano huo unafanyika wakati kukiwa na mfululizo wa maonyo ya hivi karibuni kutoka kwa watu wa ndani ya sekta hiyo kuhusu uwezo unaobadilika kwa kasi wa mifumo ya AI ya hali ya juu au "frontier AI", pamoja na kanuni zinazohitajika ili kudhibiti teknolojia hiyo.
"Watu waliounda teknolojia hizi sasa wanaonya kwamba AI iko katika hatari ya kukuza uwezo hatari zaidi" Mfalme aliwaambia viongozi hao.
Alisema kunaonekana kuwa na "dharura" ya "kuzingatia ipasavyo hatari za kuwepo zinazoweza kusababishwa na teknolojia kama hizi kuangukia mikononi mwa watu wasiofaa, na kutumiwa kwa njia zinazoweza kusababisha maafa".
"Kazi iliyo mbele yenu si kuendeleza teknolojia tu, bali kuhakikisha kwamba inabaki kutumika kwa manufaa ya binadamu, jamii na mazingira ya asili," aliwaambia washiriki wa mkutano huo.
Mkutano huo umeitishwa ili kujadili ikiwa kunaweza kuandaliwa " kanuni za pamoja" zitakazosaidia "kuongoza matumizi ya AI katika siku zijazo".
0 Comments