Olu Jacobs, mmoja wa waigizaji maarufu zaidi nchini Nigeria, ambaye taaluma yake ilidumu kwa miongo kadhaa katika nyanja za ukumbi wa michezo, televisheni na filamu, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84.
Mkewe, mwigizaji mkongwe Joke Silva, alitangaza kifo chake na kuomba faragha wakati familia ikiwa katika kipindi cha maombolezo.
Silva alitangaza kifo hicho katika taarifa iliyomwelezea mwigizaji huyo mashuhuri kama "Simba wa Lufodo" na kusema kuwa aliishi maisha yenye mafanikio na mapambano ya dhati.
Baadhi ya filamu zake mashuhuri ni pamoja na*My Kingdom, Covert Operation* na One Fine Day.
Alichukuliwa kuwa mmoja wa waanzilishi na nguzo muhimu za Nollywood kama tasnia ya filamu ya Nigeria inavyojulikana na alijipatia heshima na pongezi kubwa kote nchini.
"Tunawaomba wanablogu wote na watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii kuheshimu faragha ya familia yetu katika kipindi hiki," Silva alisema katika taarifa hiyo.
Jacobs, aliyezaliwa tarehe 11 Julai 1942, alipata mafunzo katika chuo cha Royal Academy of Dramatic Art jijini London kabla ya kuanza taaluma iliyojumuisha kushiriki katika vipindi vya televisheni vya Uingereza na filamu za kimataifa.
Baadaye, alikuja kuwa mmoja wa watu muhimu waliojenga tasnia ya filamu ya Nigeria, akishiriki katika kazi nyingi za ndani na kujipatia sifa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuigiza na uhodari wa kuigiza aina mbalimbali za wahusika.
0 Comments