Mamlaka nchini Zambia zimewaonya wananchi kutokula nyama ya wanyamapori baada ya wanyama kadhaa, wakiwemo viboko, tembo, nyati na mamba kufa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kimeta au anthrax.
Afisa wa kitengo cha kukabiliana na majanga amesema kuwa, kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita watu 12 wameambukizwa ugonjwa huo baada ya kula nyama ya wanyama pori waliokuwa wamefariki karibu na eneo la Mto Munyamadzi.
Afisa huyo amewataka raia wa taifa hilo kutokula nyama ya wanyama waliofariki kwa sababu zisizojulikana, na badala yake kuripoti visa hivyo kwa mamlaka.
Mamlaka pia zimeagiza kusitishwa kwa uwindaji hadi pale kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo utabainika baada ya uchunguzi kufanywa.
Kimeta au anthrax ni ugonjwa ambao mlipuko wake hushuhudiwa mara kwa mara nchini Zambia.
Mwaka wa 2023, Zambia ilikumbwa na kile kilichoelezwa kuwa mlipuko mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa, uliosababisha vifo vya watu wanne na kupelekea kusambaa kwa ugonjwa huo katika mikoa tisa kati ya 10 ya nchi hiyo.
Mlipuko mwingine mkubwa uliripotiwa mwaka wa 2011, ambapo zaidi ya watu 500 waliambukizwa na watu watano walifariki baada ya kula nyama ya viboko walioambukizwa.
Katika mlipuko wa sasa, Kitengo cha Zambia cha Kudhibiti na Kukabiliana na Majanga kimesema viboko 46, tembo wanane, nyati watano na mamba mmoja wamekufa tangu mwezi Julai.
0 Comments