IRINGA: Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanatarajiwa kuanza kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika baada ya kukamilika kwa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 wa Iringa–Kisada–Mbeya–Tunduma–Sumbawanga (TAZA), hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi, uwekezaji na utoaji wa huduma bora za kijamii mkoani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha Rukwa kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza, jambo litakaloongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi, taasisi za umma, viwanda na wafanyabiashara.

Akizungumza Oktoba 24, 2026 wakati wa kikao na wakandarasi wa mradi huo, Twange amewataka kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo Novemba 15, 2026 ili wananchi waanze kupata manufaa yaliyokusudiwa.

“Huu ni mradi mkubwa wa kimkakati wenye urefu wa kilomita 616 na gharama ya takribani Shilingi trilioni 2. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa katika sekta ya nishati. Kukamilika kwa mradi huu kutawapatia wananchi wa Rukwa umeme wa uhakika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi,” amesema Twange.

Amesema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 96.57 ya utekelezaji na utakapokamilika utaongeza uwezo wa Gridi ya Taifa kusafirisha umeme, kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika viwanda, madini, biashara na kilimo.

Kwa wananchi wa Rukwa, mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora katika hospitali, shule na taasisi nyingine za kijamii zinazotegemea umeme, huku ukiimarisha shughuli za uzalishaji mali na ajira kupitia uwekezaji unaotegemea nishati ya uhakika.

Aidha, Twange amesema mradi huo una umuhimu wa kikanda kwa kuwa utakamilisha maandalizi ya kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia, hatua itakayowezesha biashara ya umeme kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumzia changamoto zilizochelewesha mradi huo, amesema ni pamoja na usafirishaji wa vifaa vikubwa, hususan transfoma zenye uzito wa zaidi ya tani 200, zilizohitaji maandalizi maalum ya miundombinu ya barabara kabla ya kusafirishwa.

Hata hivyo, TANESCO inaendelea kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha vifaa vilivyosalia vinafikishwa salama katika maeneo ya mradi ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliokubaliwa.

Mradi wa TAZA, ambao awali ulitarajiwa kukamilika Mei 2026, sasa unatarajiwa kukamilika Novemba 15, 2026, ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.