Rais William Ruto

Rais William Ruto amewaamuru raia wa kigeni wanaojihusisha na shughuli za uuzaji wa bidhaa za biashara ndogo ndogo nchini Kenya kuacha, akisema serikali itachukua hatua ya kuwalinda wafanyabiashara wa ndani kutokana na ushindani usio wa haki.

Akizungumza baada ya kukutana na wafanyabiashara wa Biashara ndogo, ndogo na za Kati (MSME) katika Ikulu ya Nairobi, Jumatano, Septemba 2, Ruto alirejelea wasiwasi ulioibuka kwamba baadhi ya wageni wameanzisha biashara zinazouza bidhaa kama vile duvet na bidhaa zingine, wakishindana moja kwa moja na wachuuzi wa ndani na wafanyabiashara wadogo.

Rais alisema Muswada uliopo mbele ya Bunge hivi sasa unalenga kuwazuia raia wa kigeni kujihusisha na shughuli fulani za biashara nchini Kenya.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara na wadau wengine kujadili sheria iliyopendekezwa kabla ya kupitishwa ili kuhakikisha kwamba mianya yoyote inayowaruhusu wageni kujihusisha na biashara za uchuuzi na biashara zingine ndogo ndogo imeziba.

"Tuna Muswada Bungeni kwamba kuna baadhi ya shughuli za biashara ambazo wageni hawawezi kufanya nchini Kenya. Kwa mujibu wa sheria, nataka mketi chini na wafanyibiashara waangalie kwa sababu hatujapitisha ili tufunge mianya yote ili mtu asitoke China kuja kuwa mchuuzi," Ruto alisema.

Rais alisema kwamba hata wakati serikali inasubiri Bunge lifikirie na kupitisha sheria iliyopendekezwa, hatua za kiutawala zitachukuliwa kushughulikia raia wa kigeni wanaofanya kazi kama wachuuzi na wafanyabiashara wadogo.