Songea, Ruvuma: Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kuwa imefanya ununuzi wa gari aina ya Toyota Coaster kwa gharama ya Shilingi milioni 334, ikielezwa kuwa taarifa hizo zinalenga kupotosha umma kuhusu ununuzi wa gari hilo.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Septemba 20, 2026, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imeeleza kuwa gari hilo lenye namba za usajili STN 7615 lilinunuliwa jipya kupitia Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) kwa gharama ya Shilingi milioni 334, likiwa halijawahi kutumika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ununuzi wa gari hilo ulifanyika kwa kuzingatia taratibu za ununuzi wa Serikali na lengo lake ni kuboresha usafiri wa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wadau wa maendeleo wanapotekeleza shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.

Gari hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 30 pia linatarajiwa kupunguza matumizi ya fedha za Serikali, kwa kuwa litatumika kama mbadala wa matumizi ya magari mawili hadi matatu katika safari moja yenye idadi kubwa ya wasafiri.

Ofisi hiyo imewataka watumiaji wa mitandao ya kijamii, wadau wa habari, wanahabari na wananchi kwa ujumla kutumia uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia ukweli na uchambuzi wa jambo ili kuepusha taharuki inayoweza kusababishwa na taarifa zisizo sahihi.

Aidha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imewataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambaa mitandaoni zenye nia ya kupotosha ukweli kuhusu ununuzi wa gari hilo, na kusisitiza kuwa itaendelea kusimamia masilahi ya umma kwa uadilifu, huku ikiwataka wananchi kuwa watulivu.