Simba 10 wamekutwa wamekufa katika eneo la Ndutu, ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha, huku mamlaka zikianzisha uchunguzi wa kitaalamu kubaini chanzo cha vifo hivyo na iwapo kuna wahusika.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), mizoga ya simba hao iligunduliwa Septemba 18, 2026, katika eneo la Ndutu, Kata ya Endulen.

Uchunguzi wa awali umeonyesha uwezekano wa simba hao kufa baada ya kula au kuingiza sumu mwilini. Hata hivyo, mamlaka zinaendelea na uchunguzi ili kuthibitisha chanzo halisi cha vifo hivyo na kubaini iwapo kuna waliohusika.

NCAA imesema taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zitatolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitaalamu.

Tukio hilo limeibua wasiwasi kuhusu usalama wa wanyamapori katika eneo la Ngorongoro, ambalo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania.

Na Haika Urio | GPL -TUDACO