Rais Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa hofu kuhusu usalama wa Akili Bandia (AI) ni "uzushi", huku akikosoa wito wa kuwepo kwa hatua zaidi za udhibiti kwa teknolojia hiyo inayokua kwa kasi.

Kauli hiyo imekuja baada ya Jack Clark, mwanzilishi mwenza wa kampuni kubwa ya AI iitwayo Anthropic, kuiambia BBC kuwa huenda ikahitajika kuweka sheria ya lazima katika sekta hiyo ya kuwa na "kitufe cha kuzima" (kill switch) kwa mifumo hatari ya AI, ambacho kinaweza kukaguliwa na upande wa tatu.

Maoni ya Clark yalifuatia maonyo kuhusu hatari ambazo teknolojia hiyo inaleta kwa binadamu, maonyo yaliyotolewa hivi karibuni na watendaji pamoja na wafanyakazi kadhaa katika kampuni zinazoongoza kwenye sekta ya AI.

Hofu hizo zilisababisha mauzo makubwa ya hisa za baadhi ya kampuni za teknolojia siku ya Jumatatu, huku wawekezaji wakitathmini athari zinazoweza kutokea kutokana na uwezekano wa kupungua kwa kasi ya maendeleo ya AI.

Katika mfululizo wa machapisho kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu, Rais wa Marekani alilinganisha maonyo kuhusu AI na "Uzushi wa Kupanda kwa Joto Duniani" (Global Warming Scam), jambo ambalo alisema "linaendelezwa na Wademokrat wenye msimamo mkali wa kushoto na wapumbavu" (Radical Left Dumocrats).

Trump pia alijiita "Mvumbua Uzushi" (Hoax Buster), akilinganisha hofu kuhusu usalama wa teknolojia hiyo na kile alichokiita "Uzushi wa URUSI, URUSI, URUSI".

Katika chapisho jingine aliandika: "Kuna njama CHAFU zinazoendelea dhidi ya AI na Vituo vya Data, na pekee anayefurahia hilo ni China. YEYOTE ATAKAYESHINDA KWENYE AI, NDIYE ATAKAYESHINDA!"

Na mapema siku ya Jumatatu, Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa "hatua pekee za udhibiti" zinazohitajika kwa ajili ya AI ni kuwa na rais "imara na mwenye akili".