Mamia ya maelfu ya watu wamemlaki Papa Leo XIV katikati mwa jiji la Paris wakati wa Misa kubwa iliyofanyika uwanjani.
Umati huo ulishangilia huku kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki akipita katika Barabara ya Champs-Élysées chini ya Mnara wa Arc de Triomphe, akiwapungia mkono waumini akiwa kwenye gari maalum la kipapa.
Papa alibariki watoto kadhaa wachanga alipokuwa akisalimia waumini katika vituo mbalimbali kando ya barabara hiyo, huku sauti za watu wakipaza, "Leo, Leo", zikisikika kila upande.
Zaidi ya watu nusu milioni wanatarajiwa kushiriki hafla hiyo iliyofanyika katikati ya mji mkuu wa Ufaransa siku ya Jumamosi. Madhabahu maalum pia imejengwa katika eneo la Place de la Concorde kwa ajili ya ibada hiyo.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambaye alikutana na Papa Leo kwa mazungumzo ya saa moja siku ya Ijumaa, hatashiriki misa yoyote wakati wa ziara ya siku nne ya Papa nchini humo. Hatua hiyo inalenga kuepuka kukiuka kanuni kali za Ufaransa za kutenganisha dini na serikali.
Hata hivyo, Misa iliyofanyika Champs-Élysées itahudhuriwa na mke wa rais, Brigitte Macron, pamoja na Waziri Mkuu Sébastien Lecornu.
Baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa urais wa mwaka ujao pia wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.
0 Comments