Takriban watu 10 waliokuwa wakipanda milima kutoka Nepal na walikuwa wakijiandaa kuongoza msafara wa kupanda milima, katika milima ya Himalaya hawajulikani walipo, baada ya theluji kuporomoka na kuifunika kambi yao.

Waandaaji wa msafara huo wamesema,wapanda milima hao walikuwa katika kambi ya maandalizi, iliyopo katika eneo la Himlung, kilele cha mlima Himalaya wakati maporomoko hayo yalitokea.

Utabiri wa hali ya hewa umeonyesha kuwa, kulikuwa na maporomoko makubwa ya theluji karibu na kilele hicho chenye urefu wa mita 7,126 katika siku za hivi karibuni.

Mlima huo uko kwenye mpaka wa Nepal na Tibet.

Hali mbaya ya hewa imekwamisha juhudi za uokoaji, huku helikopta na timu za uokoaji zikishindwa kufika eneo la mkasa.

Bibhuti Chand Thakur kutoka kampuni ya Himalaya Holidays Trekking, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa “Wapanda milima wanane wa timu yetu ya kuongoza msafara na wengine wawili kutoka kampuni nyingine wameripotiwa kutoweka.”

Wilaya za milimani nchini Nepal zimekumbwa na mvua na kuporomoka kwa theluji katika siku za hivi karibuni, hali ambayo inahatarisha sekta ya utalii ya kupanda milima,ambayo ni muhimu katika uchumi wa taifa hilo.