
Watu 12 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha lori na gari la Jeshi la Polisi Tanzania, iliyotokea Septemba 21, 2026 majira ya saa moja na dakika 30 asubuhi katika Barabara ya Singida–Nzega, eneo la Milima Sekenke, Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ajali hiyo ilihusisha lori lenye namba za usajili RAF 243X/TRL 4255 mali ya Kampuni ya YYUSSA ya Kigali, Rwanda, na Toyota Land Cruiser yenye namba PT 1982 mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Ndanarasa Christian Alfonse, raia wa Rwanda, likitokea Dar es Salaam kuelekea nchini Rwanda, ambapo lililigonga gari la Jeshi la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Stafu Sajenti (S/SGT) Ussi Hassan. Gari hilo lilikuwa likitokea Kituo cha Polisi Shelui kuelekea Kiomboi kwa ajili ya kuwapeleka mahabusu mahakamani.
Waliofariki katika ajali hiyo ni askari watano wa Jeshi la Polisi, ambao ni SP Frank Lazima Mwasapili, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Shelui; S/SGT Ussi Hassan; SGT Paulo Silivin Gabriel; PC Ashraf Salumu Kheri na PC Nangida Ramadhani Mushi.
Aidha, mahabusu saba waliokuwa kwenye gari hilo pia wamefariki. Wao ni Timotheo Lazaro Kimaro na Cassian Hassan, wakazi wa Doromoni; Fred Musuguli Mzoa, Wilfred Marko Amos na Mariam Hamis Kasijao, wakazi wa Mingela, pamoja na Vivian Saidi, mke wa Nsusu, na Hussen Hussein Kea, mke wa Tulya.
Majeruhi wawili wametajwa kuwa ni Petro Organes Nkana, mke wa Mingela, pamoja na Ndanarasa Christian Alfonse, dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo. Wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Kiomboi, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mandewa, Singida.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo kuwa uzembe wa dereva wa lori, ambaye alishindwa kumudu gari lake na kuhamia upande wa kulia kisha kuligonga gari la Jeshi la Polisi na kusababisha magari yote mawili kutumbukia korongoni.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limetoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, ikiwemo hali ya hewa na miundombinu ya barabara, ili kuchukua tahadhari na kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na hasara kwa Taifa.

0 Comments