Watu 27 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya risasi yaliyotokea nchini Afrika Kusini.
Watu 17 waliuawa baada ya wanaume wanane waliojihami na bunduki kuvamia baa moja karibu na mji Johannesburg jana jioni, huku wengine 15 wakijeruhiwa.
Katika tukio tofauti lililotokea mapema leo asubuhi, watu 10 wameuawa nje ya eneo la burudani karibu na mji Cape Town, huku wengine 11 wakijeruhiwa.
Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi vya mauaji kutokana na uhalifu duniani, na katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kudhibiti ghasia zinazohusishwa na magenge na matumizi ya bunduki.
Polisi bado hawajathibitisha sababu za mashambulizi hayo mawili kufanyika.
Mjini Johannesburg, watu waliojihami kwa bunduki waliwafyatulia risasi wateja waliokuwa nje ya baa hiyo kabla ya kuingia ndani na kuendelea na mashambulizi. Pia walichoma moto magari mawili kabla ya kutoroka.
Polisi walisema wanaume 13 na wanawake wanne waliuawa, huku sababu ya shambulizi hilo ikiwa bado hakijabainika.
Huko Cape Town, waathiriwa watano walifariki katika eneo la tukio, huku wengine watano wakifariki hospitalini.
Mashambulizi hayo mawili ya risasi yametokea siku chache tu baada ya watu 11 kuuawa mjini Durban, baada ya watu wenye bunduki kuvamia nyumba moja katika mtaa wa KwaMakhutha.
Kufikia leo asubuhi, bado polisi hawajafanikiwa kuwakamata washukiwa.
0 Comments