Na Mwandishi Wetu- Same

Katibu Tawala Wilaya ya Same Bi. Mamndolwa Gembe amewataka Kamati ya Usimamizi wa Maafa Wilaya ya Same kuendelea kutoa elimu ya tahadhari kwa wananchi wa maeneo yote ya wilaya hiyo hususani wakulima na wafugaji.

Bi. Gembe amesisitiza hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, leo Octoba 06, 2026, wakati akifungua kikao kazi cha Kamati za usimamizi wa maafa za wilaya na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) sambamba na kuimarisha utoaji wa matumizi ya taarifa za tahadhari za awali katika kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El nino.


“Wilaya ya Same ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabianchi, kijiografia wilaya yetu ina maeneo ya milima na tambarare, hivyo inatufanya tuwe katika hatari ya kukabiliwa na changamoto za pande mbili, kutokana na hilo mipango na mapendekezo yatakayotolewa katika kikao kazi hiki yasibaki kwenye nyaraka tu, bali yakatimizwe na kuingizwa kwenye mipango kazi ya halmashauri, mamlaka za kata na vijiji” amesisitiza Bi. Gembe.

Aidha, Bi. Gembe ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa ushirikiano lakini pia amesema kuwa Serikali ya Wilaya ya Same ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega ili kuhakikisha malengo ya programu hiyo yanatimia.

“Tunawashukuru sana kwa kuchagua Wilaya ya Same kuwa sehemu yay a ziara na kikao kazi hiki cha kimkakati, ujio wenu ni Ushahidi tosh awa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kulinda Maisha na mali za wananchi dhidi ya athari za majanga Ameongeza Katibu Tawala huyo.

Nae, Mwakilishi kutoka Shirika la Chakula Duniani (WFP) Bi. Sandra Hakim amebainisha kuwa, lengo la programu hiyo ni kuifanya taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa inashuka chini ili jamii ikiwemo wazee, wamama, walemavu na watoto waweze kupata taarifa kwa wakati kwani upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa mapema zitakuwa na thamani pale utakapochukua hatua kabla ya majanga kutokea.

Katika kikao hicho mada mbalimbali kuhusu Utabiri wa Msimu, El nino na madhara tarajiwa, Dhana ya Maafa ikiwemo mzingo wa maafa, Mpango wa Dharurawa Kukabiliana na Maafa na majukumu ya kamati na utekelezaji wa mpango pamoja na Usambazaji wa Huduma za Hali ya Hewa ziliwasilishwa kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa.