Kundi la mataifa saba yenye uchumi mkubwa duniani (G7) limetangaza kuwa litaachia soko mapipa milioni 100 ya mafuta ghafi na dizeli, katika juhudi za kupunguza hofu kuhusu upatikanaji wa nishati ambayo imechangia kupanda kwa kasi kwa bei za mafuta.

Viongozi wa G7 walisema katika taarifa kwamba hatua hiyo itahusisha kutolewa kwa kiasi kikubwa cha dizeli kwenye soko katika kipindi cha siku 20 zijazo. Pia walibainisha kuwa akiba zaidi ya dizeli itaachiliwa endapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

Kundi hilo, linalojumuisha Marekani, Uingereza, Canada, Japan, Ujerumani, Italia na Ufaransa, limesema hatua hiyo itaanza kutekelezwa mara moja na itaendelea kwa kipindi cha miezi minne. Umoja wa Ulaya pia hushiriki katika mikutano ya G7.

Tangazo hilo limekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia kupiga marufuku usafirishaji wa dizeli ya Marekani kwenda mataifa mengine iwapo nchi za Ulaya zisingekubali kutoa sehemu ya akiba zao za mafuta.

Chini ya makubaliano hayo mapya, hakutakuwa na vikwazo vya usafirishaji wa nishati na bidhaa zinazohusiana na nishati kati ya nchi wanachama wa G7.

Trump alisema hatua ya Ulaya kukubali kuachia sehemu ya akiba yake ya dizeli itasaidia kutuliza soko la nishati.

"Ulaya sasa imekubali kutoa kiasi kikubwa cha akiba yake ya ziada ya dizeli. Mchakato huu utaanza mara moja," Trump alisema kupitia mitandao ya kijamii siku ya Ijumaa.

Awali, Trump alikuwa ameonya kwamba angezuia usafirishaji wa dizeli ya Marekani kwenda nje ya nchi. Hatua kama hiyo ingeweza kupunguza shinikizo la bei kwa walaji wa Marekani kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba, lakini pia ingesababisha bei ya mafuta kupanda katika mataifa mengine yanayotegemea usambazaji wa Marekani.

Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, alisema wakulima, madereva wa malori na wafanyabiashara nchini humo hawapaswi kubeba mzigo mkubwa wa kupanda kwa bei za nishati wakati nchi nyingine zina akiba inayoweza kusaidia kutuliza soko.