
DAR ES SALAAM. TANZANIA imepata kibali FIFA kuendelea kutumia mfumo wa msaada wa video kwa waamuzi (Football Video Support (FVS), huku Ligi Kuu ikitajwa kuwa ya kwanza duniani kutumia mfumo huo kwa utaratibu uliokubaliwa na Shirikisho hilo la Kimataifa la Soka (FIFA).
Akizungumza Dar es Salaam leo Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Cornel Barnabas, amesema mfumo huo umekuwa ukisaidia kupunguza makosa ya waamuzi na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wakati wa michezo.
Amesema baada ya kutumia mfumo huo kwa kipindi, Bodi ya Ligi iliendelea na taratibu mbalimbali kwa kushirikiana na FIFA ili kuhakikisha matumizi yake yanafanyika katika mazingira bora na kwa kuzingatia taratibu za kimataifa.
“Tumekuwa tukitumia Football Video Support katika kupunguza au kuwasaidia waamuzi wetu kufanya maamuzi sahihi. Katika kipindi chote tumeona mafanikio ambayo yamejitokeza,” amesema Barnabas.
Amesema kwa kushirikiana na FIFA wamekamilisha taratibu hizo na kupata kibali cha kuendelea kutumia mfumo huo kitaalamu zaidi, huku Tanzania ikiendelea kushirikiana na shirikisho hilo katika kuboresha matumizi yake.
Barnabas amesema Ligi Kuu ina jumla ya mechi 240 kwa msimu, ambapo kati ya hizo, mechi 150 zitachaguliwa na kuwasilishwa taarifa kwa FIFA, ikiwemo namna mfumo huo ulivyotumika katika michezo hiyo.
Amesema utaratibu huo utaanza katika mchezo ujao wa Debi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba, utakaochezwa Oktoba 10, kwenye Uwanja wa Uhuru kabla ya kuendelea katika michezo mingine itakayochaguliwa kati ya 240 ya ligi.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika soka la Tanzania na kuhakikisha mfumo huo unaendelea kuwa msaada kwa waamuzi katika kufanya maamuzi sahihi wakati wa mechi.
0 Comments