Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ameomba radhi kwa Baraza la FIFA kufuatia dosari katika mawasiliano na mashauriano kuhusu mpango wa Fifa Forward Enterprise (FFE), uliopendekeza kuhamisha sehemu ya haki za kibiashara za FIFA kwa kampuni binafsi ya uwekezaji.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la FIFA wamesema msamaha huo haujajibu maswali muhimu yaliyopo. Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England (FA) na Makamu Rais wa FIFA, Debbie Hewitt, amesema Infantino anapaswa kuweka wazi nyaraka zote zinazohusiana na mpango huo na kutoa majibu ya kina kuhusu masuala yaliyozua utata.
Hewitt alisisitiza kuwa ikiwa Infantino hatafanya hivyo, atakuwa ameshindwa kuonyesha sifa zinazostahili kwa kiongozi wa FIFA. Aliongeza kuwa uwazi kuhusu mpango wa FFE na maamuzi mengine yenye utata ndani ya FIFA ni muhimu ili kurejesha imani ya viongozi wa soka duniani.
Kwa upande wake, Infantino amesema FFE ilikuwa pendekezo tu na si uamuzi uliokuwa umekamilika, akiahidi kuyajibu maswali yaliyosalia kwa maandishi.
Wakati huohuo, UEFA imeendelea kuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Infantino, ikisisitiza kuwa nyaraka zote zinazohusiana na mpango huo zinapaswa kuwekwa wazi ili kubaini kilichotokea na kama kulikuwa na ukiukwaji wowote wa taratibu.

0 Comments