Mwanasheria wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, amesema Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, anatarajia kuanza mgomo wa kula Jumatatu, Oktoba 26, 2026, kupinga kunyimwa haki ya kufanya mazungumzo ya faragha na mawakili wake.

Akizungumza katika makao makuu ya CHADEMA, Mikocheni, Dar es Salaam, Oktoba 24, Dkt. Nshala amesema hatua hiyo inatokana na kile alichokitaja kuwa ni kutoheshimiwa kwa uamuzi wa Mahakama ulioruhusu Lissu kuzungumza na mawakili wake kwa faragha.

Dkt. Nshala ameongeza kuwa Lissu amedhamiria kuanza mgomo huo na kusitisha matumizi ya dawa kuanzia Jumatatu, kama njia ya kushinikiza mamlaka kuheshimu haki zake za kisheria.

Akirejelea Katiba ya Tanzania, Ibara ya 26(1), Dkt. Nshala amesema kila mtu ana wajibu wa kutii Katiba na sheria za nchi, akiwemo kila aliyepewa jukumu la kuzisimamia.

Amehoji kwa nini sheria hazizingatiwi, akisema: “Je, tunakwenda wapi kama nchi? Kwa nini tunafika hapo? Kwa nini tunasema tuko chini ya sheria, lakini sheria hazifuatwi bila masharti?”

Dkt. Nshala amedai kuwa kutotekelezwa kwa uamuzi wa Mahakama kunazua wasiwasi kuhusu utawala wa sheria nchini, akisema sheria zinaonekana kutumiwa kwa namna tofauti, ikiwemo kukandamiza wanaopinga au kukosoa walio madarakani.

Kuhusu afya ya Lissu iwapo ataanza mgomo wa kula na kusitisha matumizi ya dawa, Dkt. Nshala amesema suala hilo linaachiwa wananchi kulitafakari.

Haya yanajiri baada ya Mahakama kusema itahitaji muda wa kutosha ili iweze kutoa maamuzi sababu kesi inayomkabili Lissu ni shauri la namna yake.

Watanzania wanasubiri kujua hukumu itakayotolewa dhisi ya Lissu iliyoartibiwa kufanyika tarehe sita mwezi wa kumi na moja saa tatu asubuhi.