Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi Mwezi wa Huduma kwa Wateja 2026 kwa kusisitiza dhamira yake ya kwenda hatua ya ziada katika kuwafikia wateja kwenye maeneo yao ya biashara na shughuli za kiuchumi, kusikiliza mahitaji yao na kutumia mrejesho huo kuboresha huduma na suluhisho za kifedha.


Mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu “Extra Mile – Hatua ya Ziada,” inayolenga kuakisi dhamira ya NBC kwenda zaidi ya utoaji wa huduma za kawaida kwa kuelewa mahitaji ya mteja, kufuatilia changamoto hadi zinapatiwa ufumbuzi na kuendelea kubuni huduma zinazorahisisha maisha na biashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NBC, Bi. Alelio Lowassa, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi, alisema Extra Mile si kaulimbiu ya mwezi mmoja bali ni sehemu ya utamaduni wa huduma ambao NBC inalenga kuutekeleza kila siku.

“Kwetu NBC, Extra Mile si kaulimbiu ya mwezi mmoja. Ni namna tunavyotaka kuwahudumia wateja wetu kila siku. Ni kusikiliza na kuelewa hitaji la mteja, kufuatilia jambo hadi lipatiwe ufumbuzi, kuheshimu muda wa mteja, kutimiza ahadi zetu na kuendelea kubuni huduma zinazorahisisha maisha na biashara za wateja wetu,” alisema.

Bi. Lowassa alisema NBC imeamua kuendesha maadhimisho hayo kwa mwezi mzima ili kupata muda zaidi wa kusikiliza wateja, kujifunza na kuboresha huduma, huku ikiendelea kuwekeza katika teknolojia na kupanua mtandao wa huduma ili kukidhi matarajio ya wateja wanaohitaji huduma zenye kasi, usalama na urahisi.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita NBC imefungua wastani wa matawi matano mapya kila mwaka, huku mtandao wa NBC Wakala ukifikia zaidi ya mawakala 26,000 nchini. Aidha, benki hiyo imeendelea kuboresha NBC Kiganjani, NBC Connect, GePG na NBC Lipa Namba, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa mikopo ikiwemo mikopo ya muda mfupi ya hadi siku 30 kupitia NBC Kiganjani.

“Lengo ni moja: kupunguza muda na hatua anazotumia mteja kupata huduma. Hii ndiyo maana ya ahadi yetu ya Daima Karibu Nawe,” alisema.

Hafla hiyo pia ilihusisha mjadala maalum wa jopo (panel discussion) uliowakutanisha wateja wa NBC pamoja na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali, waliopata fursa ya kujadili uzoefu wao na mchango wa huduma za kifedha katika kukuza shughuli za kiuchumi.

Akizungumza kwenye mjadala huo, Mkuu wa Idara ya Bima wa NBC, Bw. Benjamin Nkaka, alionyesha kuridhishwa na kasi ya ongezeko la makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo wakulima, kutumia huduma za bima, ikiwemo bima ya afya na kilimo, hali inayochangiwa na kuongezeka kwa elimu kuhusu umuhimu wa bima na utayari wa jamii kukabiliana na hatari zinazoweza kuathiri shughuli zao za uzalishaji.

“Zaidi kwa sasa tunaelekea kwenye mvua za El Niño na Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamewekeza nguvu katika kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari, hususani kwenye maeneo ya miundombinu na mahitaji mengine muhimu ikiwemo chakula. Sisi wadau wa bima tunaunga mkono jitihada hizo kwa kuwahamasisha wananchi wawekeze pia kwenye bima ili waweze kupata ulinzi wa mali zao pindi watakapokumbana na athari za mvua hizo, ili kulinda mitaji, mazao, mifugo na biashara zao,” alisisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya wateja wengine wa benki hiyo, mfanyabiashara na mteja wa muda mrefu wa NBC, Bw. Assaa Simba Haroun, aliipongeza benki hiyo kwa hatua ya kuwafikia wateja kwenye maeneo yao, akisema wafanyabiashara wanahitaji uangalizi na ushauri wa karibu kutoka taasisi za fedha ili kuwawezesha kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kulinda mitaji yao.

“Hatua hii ya NBC kuwatembelea wateja wake inakwenda kuondoa changamoto ya muda mrefu inayowakabili wafanyabiashara wengi ambao baada ya kukopeshwa tu taasisi za fedha huwa zinawaacha bila uangalizi wowote hadi pale mambo yanapokwenda kombo. Tunawapongeza sana NBC kwa mkakati huu muhimu unaolenga kuwalea wafanyabiashara wasiwe wapweke dhidi ya changamoto zinazowakabili,” alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu maadhimisho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa NBC, Bi. Salama Mussa, aliwashukuru wateja kwa muitikio wao kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo, huku akiwataka wafanyakazi wa NBC kutumia maadhimisho hayo kuwafikia wateja kwenye maeneo yao, kutatua changamoto za kihuduma na kuendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali ili kuwawezesha kupata huduma kwa kasi, usalama na urahisi zaidi.


Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Bi. Alelio Lowassa (kushoto), akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwezi wa Huduma kwa Wateja wa NBC, iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo, wafanyakazi pamoja na wateja wa NBC.

Mkurugennzi wa Biashara wa NBC, Bw Jacob Kashimba (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwezi wa Huduma kwa Wateja wa NBC, iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo, wafanyakazi pamoja na wateja wa NBC.

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo, Elibariki Masuke (alieshika mic) akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwezi wa Huduma kwa Wateja wa NBC, iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo, wafanyakazi pamoja na wateja wa NBC.

Akizungumza kwenye mjadala huo, Mkuu wa Idara ya Bima wa NBC, Bw. Benjamin Nkaka (alieshika mic) alionyesha kuridhishwa na kasi ya ongezeko la makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo wakulima, kutumia huduma za bima, ikiwemo bima ya afya na kilimo, hali inayochangiwa na kuongezeka kwa elimu kuhusu umuhimu wa bima na utayari wa jamii kukabiliana na hatari zinazoweza kuathiri shughuli zao za uzalishaji.

Meneja Mawasiliano na Mahusiano ya Umma Mwandamizi wa benki ya NBC Bi Brendansia Kileo akiongoza mjadala wa wataalam wabobezi (panel discussion) wakati wa hafla wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwezi wa Huduma kwa Wateja wa NBC, iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo, wafanyakazi pamoja na wateja wa NBC.

Akizungumza kwa niaba ya wateja wengine wa benki hiyo, mfanyabiashara na mteja wa muda mrefu wa NBC, Bw. Assaa Simba Haroun (pichani) aliipongeza benki hiyo kwa hatua ya kuwafikia wateja kwenye maeneo yao, akisema wafanyabiashara wanahitaji uangalizi na ushauri wa karibu kutoka taasisi za fedha ili kuwawezesha kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kulinda mitaji yao.

Katika hafla hiyo wateja wa benki ya NBC walipata wasaa kutoa maoni yao kuhusu huduma mbalimbali za benki hiyo.




Baadhi ya wateja wakifuatilia hafla hiyo.

Hafla hiyo ilihusisha maofisa waandamizi wa benki ya NBC na wateja wa benki ya NBC.