Mahakama Kuu ya Tanzania imeuagiza uongozi wa Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam kuhakikisha unazingatia kanuni za uendeshaji wa magereza kwa kuruhusu Mawakili na washauri wa kisheria kukutana na wateja wao bila kuingiliwa au kusikilizwa mazungumzo yao.

Mahakama hiyo imesisitiza kuwa maofisa magereza wanapaswa kusimamia usalama wakati wa mazungumzo hayo kwa kukaa umbali unaowawezesha kuwaona wakili na mteja wake, lakini bila kusikia mazungumzo yao.

Maagizo hayo yametolewa leo, Oktoba 16, 2026, na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, katika shauri namba 7300/2026 lililofunguliwa na Wakili Kulwa Maduhu na wenzake, ambao ni Mawakili na washauri wa kisheria wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Katika shauri hilo, waombaji walilalamikia kuzuiwa kukutana na mteja wao pamoja na kukosekana kwa usiri wakati wa mazungumzo katika nyakati ambazo waliruhusiwa kuonana naye.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Amir Mruma, aliyekuwa kiongozi wa jopo la majaji watatu waliosikiliza shauri hilo, amesema uongozi wa Gereza la Ukonga unapaswa kufuata kanuni zinazotaka maofisa magereza kusimamia usalama bila kuvunja haki ya usiri kati ya wakili na mteja wake.

Mahakama imetamka kuwa kitendo cha maofisa magereza kusikiliza mazungumzo kati ya Lissu na Mawakili wake, Paul Kisabo na Nashon Nkungu, kinakiuka Kanuni ya 13 ya Uendeshaji wa Magereza ya mwaka 1968.

Katika uamuzi huo, Mahakama imeeleza kuwa kanuni hiyo inataka mashauriano kati ya mfungwa na wakili au mshauri wake wa kisheria yafanyike katika mazingira ambayo maofisa magereza wanaweza kuwaona, lakini wasiweze kusikia mazungumzo yao.

Aidha, Mahakama imeeleza kuwa kuzuiwa kwa Wakili Maduhu kuingia Gereza la Ukonga Oktoba 28, 2025, licha ya kuonyesha kitambulisho chake cha uwakili, kwa madai kuwa hakuwa kwenye orodha ya Mawakili iliyowasilishwa na Lissu gerezani hapo, hakukuwa na sababu inayojitosheleza.

Mahakama imesema kuwa nafasi ya Maduhu kama wakili na mshauri wa kisheria wa mteja wake, pamoja na sababu zilizokuwepo za kutaka kukutana naye, zilipaswa kuzingatiwa.

Kupitia uamuzi huo, Mahakama imewaagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Jenerali wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Ukonga kuhakikisha Mawakili wa Lissu wanapofika gerezani hapo wanaruhusiwa kukutana na kufanya mashauriano na mteja wao bila kuingiliwa kwa namna yoyote ile wala kusikilizwa mazungumzo yao.

Uamuzi huo unaweka msisitizo katika utekelezaji wa kanuni za magereza zinazolenga kulinda usalama wa wafungwa huku zikiheshimu usiri wa mawasiliano kati ya mawakili na wateja wao.