DAR ES SALAAM — Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo, amewaondoa hofu wananchi wanaopelekwa kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, akisema hospitali hiyo ina madaktari bingwa na wabobezi pamoja na vifaa tiba vya kisasa.

Dkt. Kimambo amesema Mloganzila ni tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwamba ina wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa wanaopelekwa hospitalini hapo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Delilah Kimambo.

Akijibu swali kuhusu imani ya baadhi ya wananchi kwamba Mloganzila ina wanafunzi wa udaktari wanaowahudumia wagonjwa, Dkt. Kimambo amesema dhana hiyo si sahihi.

Amesema baadhi ya wananchi huenda wakawachukulia madaktari hao kuwa wanafunzi kutokana na umri wao mdogo, wakati ukweli ni kwamba wengi wao ni madaktari bingwa na wabobezi.

“Watu wanapowaona madaktari vijana wadogo wanaamini ni wanafunzi, lakini si kweli. Ni mabingwa na wabobezi. Watu wana imani za kizamani kwamba wanatarajia kuwaona madaktari wenye umri mkubwa, lakini nawahakikishia kwamba ni vijana wabobezi,” amesema Dkt. Kimambo.

Dkt. Kimambo pia amesema Hospitali ya Mloganzila imewezeshwa kwa vifaa tiba vya kisasa vinavyoiwezesha kutoa huduma za afya za kibingwa kama ilivyo Muhimbili Upanga.

Watangazaji wa Global TV na Global Radio Elvan Sitambuli (kushoto) na Godfrey Nathan (kulia) wakiongea na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo (katikati).

Amesema miundombinu na vifaa vilivyopo hospitalini hapo vinawawezesha madaktari kutoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa bila wananchi kuwa na hofu wanapoelekezwa kupata matibabu Mloganzila.

“Hiki chumba cha upasuaji cha kisasa cha Muhimbili kipo pia Mloganzila. Ni hospitali yenye vifaa tiba kama Muhimbili, kwa hiyo watu wasiwe na wasiwasi wakipelekwa kule kutibiwa. Madaktari na vifaa vimekamilika,” amesema.

Dkt. Kimambo amesisitiza kuwa wananchi wanaopelekwa Mloganzila wanapaswa kuwa na imani na huduma zinazotolewa, kwa kuwa hospitali hiyo ni sehemu ya Muhimbili na ina wataalamu pamoja na teknolojia zinazohitajika katika utoaji wa huduma za afya.

Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutoa huduma kupitia vituo vyake vya Muhimbili Upanga na Mloganzila, huku wagonjwa wakielekezwa katika kituo kulingana na aina ya huduma wanayohitaji.

Stori na Elvan Stambuli, Global Digital | GPL