
MOROGORO: WAKULIMA nchini na wadau wa mnyororo wa thamani wa zao la mpunga wametakiwa kuangalia fursa za kuongeza thamani ya zao hilo kupitia utafiti, uchakataji na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali, badala ya kutegemea zaidi mchele kama chakula cha kawaida.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Mussa Ali Mussa, ametoa rai hiyo wakati akifungua kikao kazi cha kuthibitisha na kusaini makubaliano ya pamoja ya maendeleo ya Sekta ya Mchele kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Dk. Mussa amesema Mkoa wa Morogoro una uwezo mkubwa katika uzalishaji wa mpunga, ambapo kwa mwaka huzalisha hadi tani milioni 1.2, huku uzalishaji wa nchi ukikadiriwa kufikia tani milioni nane.
Amesema hali hiyo inaonesha umuhimu wa wataalamu kufanya utafiti wa kutosha kuhusu uwezekano wa kutengeneza bidhaa nyingine kama sabuni na mvinyo kwa kutumia mchele kama malighafi.
“Utafiti wa kutosha unaweza kusaidia kubaini bidhaa zinazoweza kuzalishwa kibiashara, kuongeza thamani ya zao hilo na kutoa fursa za uwekezaji na ajira,” amesema Dk. Mussa.

Aidha, Dk. Mussa amewataka wadau wa mnyororo wa thamani wa zao la mpunga kusaidia kuhakikisha Mkoa wa Morogoro unakuwa na maghala ya kutosha ya kuhifadhi mpunga, akisema yaliyopo ni madogo na hayatoshi.
Naye Mwakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), John Kapufi, amesema mamlaka hiyo inapanga kuimarisha usimamizi wa aina za mchele kulingana na mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kapufi amesema sifa kama harufu, ukubwa wa punje na ubora zinapaswa kuzingatiwa ili bidhaa zinazozalishwa zikidhi viwango vinavyotambulika sokoni.
Ameongeza kuwa usimamizi wa ubora utaenda sambamba na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji, uhifadhi na uchakataji wa mazao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mchele Tanzania, Geoffrey Rwiza, amesema gharama kubwa za uzalishaji na biashara zinahitaji hatua za pamoja, zikiwemo kuboresha upatikanaji wa mikopo, mbegu bora, pembejeo na zana za kilimo.
Rwiza amesema wakulima pia wanahitaji kuacha kuchanganya aina tofauti za mchele kwenye gunia moja, kwa kuwa hali hiyo inadhoofisha utambulisho wa bidhaa na kuathiri thamani yake sokoni.

Naye Mkuu wa Korido ya Ukanda wa Ukuaji wa Kilimo Tanzania (AGCOT), John Banga, amesema makubaliano ya hiari ya wadau yanaweka msingi wa kuwajibika kwa pamoja katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya mpunga.
Banga amesema kila mdau anapaswa kuwa na jukumu linaloeleweka pamoja na muda wa kutekeleza maazimio yaliyokubaliwa.
Awali, Ofisa Programu wa Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira Asilia (IUCN), Samwel Kajiba, amesema ushirikiano na AGCOT tangu mwaka 2014 umelenga kuongeza tija katika kilimo huku ukihifadhi mazingira.
Kajiba amesema kupitia mradi wa Sustain katika maeneo ya Morogoro na Iringa, unahimiza mifumo endelevu ya uzalishaji, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika na uhifadhi wa bioanuwai.
Kikao kazi hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano kati ya AGCOT na IUCN na kimewakutanisha washiriki kutoka Mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya.
0 Comments