MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameliomba Bunge kuangalia upya sheria na taratibu za manunuzi ili kurahisisha upatikanaji wa fedha na vifaa vya miradi ya maendeleo, akisema ucheleweshaji wake unasababisha miradi kutokamilika kwa wakati.
Nyongo alitoa ombi hilo Oktoba 6, 2026, baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa katika Kata ya Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe.
Alisema moja ya changamoto zinazokwamisha kasi ya ujenzi wa chuo hicho ni ucheleweshaji wa fedha pamoja na taratibu za manunuzi, hali inayosababisha baadhi ya kazi kusuasua.
“Kuna umuhimu wa kurahisisha mchakato wa manunuzi pale fedha za mradi zinapokuwa tayari, ili utekelezaji uweze kwenda kwa kasi na miradi ikamilike kwa wakati,” alisema Nyongo.
Alieleza kuwa ujenzi wa chuo hicho ulitarajiwa kukamilika mwaka 2023, lakini umekumbwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha kuchelewa, huku akipongeza kasi ya utekelezaji iliyopo kwa sasa.
Nyongo alisema kuongezeka kwa viwanda wilayani Kisarawe kunahitaji uwepo wa vijana wenye ujuzi wa ufundi, hivyo kukamilika kwa chuo hicho kutasaidia kuzalisha wataalamu watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira na viwanda vinavyoendelea kuanzishwa wilayani humo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Saidi Masoud Kisiki, alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa majengo tisa.
“Ujenzi umefikia asilimia 68.3, huku kazi katika majengo manane ikiwa imesimama kusubiri vifaa ambavyo mchakato wa manunuzi yake unaendelea katika ngazi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST),” alisema.
Aliongeza kuwa mradi huo pia unakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji, barabara na umeme.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, alisema tayari wamewasiliana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhusu changamoto ya barabara inayoelekea chuoni hapo na kwamba hatua za kuishughulikia zinaendelea.
Magoti alisema kukamilika kwa chuo hicho kutakuwa na manufaa makubwa kwa vijana wa Kisarawe kwa kuwa kitawapa fursa ya kupata elimu ya ufundi na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.
Naye Mbunge wa Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, alisema vyuo vya VETA vina nafasi muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuwapatia elimu ya vitendo na ujuzi unaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa au kuajiri wengine.
Jafo alisema chuo hicho ni fursa kubwa kwa vijana wa Kisarawe kupata ujuzi katika fani mbalimbali na kutumia ujuzi huo kujikwamua kiuchumi.


.jpeg)
.jpeg)
0 Comments