NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Kinyasi Ole Millya, amewataka wakazi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kuthamini na kuheshimu uteuzi unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan badala ya kubeza nafasi wanazopewa viongozi kutoka wilayani humo.
Ole Millya, ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro, ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Kimotorok, Kata ya Loiborsiret, alipokutana na wananchi, kuwashukuru kwa ushirikiano wao na kusikiliza kero zinazowakabili.
Amesema tangu kuanzishwa kwa Wilaya ya Simanjiro, haijawahi kupata kiongozi katika nafasi ya Naibu Waziri, hivyo wananchi wanapaswa kuthamini nafasi hiyo na kushukuru kwa hatua iliyofikiwa.
“Wana Simanjiro, tukipata nafasi ya uteuzi hata kama ni ndogo, tunapaswa kushukuru kwa moyo mkunjufu na siyo kuibeza,” amesema Ole Millya.
Akizungumzia suala hilo, Diwani wa Kata ya Komolo, Saning'o Somii, amesema baadhi ya viongozi wastaafu wanapotosha jamii kwa kudai kuwa nafasi ya Naibu Waziri ni ndogo ikilinganishwa na nafasi ya Mkuu wa Mkoa ambayo baadhi yao waliwahi kushikilia.
“Mtu badala ya kukaa pembeni baada ya kukosa uongozi, anataka kwenye sherehe aimbiwe wimbo wa sifa kama yupo madarakani,” amesema Somii.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Terrat, Jackson Ole Materi, amewataka viongozi wastaafu kujiepusha na kauli zinazoweza kudhoofisha heshima ya viongozi waliopo madarakani na badala yake kuwaachia nafasi ya kutekeleza majukumu yao.
Amesema nafasi ya Naibu Waziri ina majukumu yanayohusisha masuala ya kitaifa na ushiriki katika shughuli za Baraza la Mawaziri, huku Mkuu wa Mkoa akisimamia shughuli za Serikali katika eneo lake la kiutawala.
“Mtu anasema yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa ni nafasi kubwa kuliko nafasi ya Naibu Waziri, jambo ambalo siyo sahihi, kwani Naibu anazunguka nchi nzima na Mkuu wa Mkoa anaongoza mkoa mmoja, pia Naibu anakuwepo kwenye Baraza la Mawaziri tofauti na RC,” amesema Ole Materi.
Naye mkazi wa Kijiji cha Kimotorok, Nai Mollel, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Ole Millya kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Ningemuona mama yetu Samia ningemkumbatia na kumbusu mara 10 kama ishara ya kumshukuru kwa kumteua kuwa Naibu Waziri mtoto wetu Ole Millya,” amesema Mollel.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Wambura Igembya, amewataka wakazi wa Loiborsiret kuepuka siasa zisizo za kistaarabu na kuelekeza nguvu zao katika shughuli za maendeleo.
Naye Diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekia Lesenga maarufu kama Mardadi, amempongeza Ole Millya kwa juhudi zake za kushughulikia migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Simanjiro.
Mardadi amesema katika kipindi cha kwanza cha ubunge wa Ole Millya, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, mawaziri wanane walifika katika kata hiyo kwa lengo la kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiikabili jamii.

0 Comments