Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema maandalizi ya hafla ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, yamekamilika.


Profesa Mkumbo ameyazungumza hayo leo katoka uwanja wa mashujaa Mtumba leo ambapo amesema maandalizi hayo yamekamilika huku shughuli za uzinduzi zikitarajiwa kuanza rasmi usiku wa leo, Oktoba 29, 2026, kwa matukio mbalimbali yatakayoashiria kuanza kwa hafla hiyo muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi.

Ameeleza kuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika usiku wa leo ni upigaji wa fataki, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha hatua hiyo ya maendeleo na kuandaa mazingira ya shughuli kuu za uzinduzi zinazotarajiwa kufanyika kesho.

Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, shughuli za kesho zitahusisha matukio makuu matatu, yakianza na uzinduzi wa barabara za lami zinazounganisha maeneo mbalimbali ndani ya Mji wa Serikali Mtumba, hatua inayolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri na kurahisisha shughuli za kiutendaji katika eneo hilo.

Tukio la pili litakuwa uzinduzi wa jengo la Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, litakalowakilisha majengo mengine ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali yaliyojengwa katika Mji wa Serikali.

Tukio la tatu litakuwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Watanzania. Hotuba hiyo inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya hafla hiyo, itakayoweka alama katika hatua za kuimarisha mazingira ya utendaji wa Serikali kupitia miundombinu ya kisasa ya kiutawala.

Aidha, Profesa Mkumbo amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kushiriki hafla hiyo, akisisitiza umuhimu wa Mji wa Serikali Mtumba kama alama ya maendeleo ya nchi. Uzinduzi huo unaashiria hatua muhimu katika uwekezaji wa Serikali kwenye miundombinu ya ofisi na barabara, kwa lengo la kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali.