Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya kimataifa ya kulinda bioanuai lazima iambatane na hatua halisi, fedha endelevu na ushiriki wa jamii ili kuhakikisha mifumo ya ikolojia inalindwa, inarejeshwa na kutumiwa kwa njia endelevu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Oktoba 2026, Jijini Yerevan, Armenia, alipohutubia Mkutano wa Viongozi kuhusu Bioanuai (Leaders’ Summit on Biodiversity) COP17, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema Tanzania imeandaa Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Bioanuai wa mwaka 2025–2030, unaolenga kuimarisha uhifadhi, urejeshaji wa mifumo ya ikolojia na matumizi endelevu ya rasilimali za kibiolojia.

Akieleza hatua zilizofikiwa Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema maeneo ya hifadhi za bahari yameongezeka kutoka matano hadi saba, huku eneo linalosimamiwa kwa uhifadhi likiongezeka kutoka takriban kilomita za mraba 2,400 hadi zaidi ya 3,600, hatua inayochangia kulinda rasilimali za bahari na kukuza maendeleo endelevu.

Katika mkutano huo, Tanzania imeeleza kuunga mkono matokeo madhubuti ya kisiasa na utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya bioanuai kuelekea mwaka 2030, ikiwemo lengo la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya ardhi na bahari ifikapo mwaka huo.

Katika ujumbe wa Tanzania, Rais Dkt. Mwinyi ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya; Balozi wa Tanzania nchini Urusi anayewakilisha pia Armenia, Mhe. Fredrick Ibrahim Kibuta; pamoja na viongozi na maafisa mbalimbali wa Serikali.