MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amepiga marufuku tabia ya wanafunzi kufukuzwa au kurudishwa nyumbani kwa kushindwa kuchangia chakula shuleni, akiwataka walimu kuacha kuwaadhibu watoto kwa makosa yanayohusiana na wazazi wao.
Nyongo alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika Kata ya Msata, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, alipokutana na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero zao.
Alisema mtoto hapaswi kunyimwa fursa ya kupata elimu kwa sababu mzazi au mlezi ameshindwa kutimiza mchango wa chakula, akisisitiza kuwa walimu wanapaswa kufuata utaratibu unaofaa katika kushughulikia changamoto hizo bila kumuathiri mwanafunzi.
Hata hivyo, Nyongo aliwataka wazazi na walezi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni, akieleza kuwa pamoja na Serikali kutoa elimu bila ada, jamii ina wajibu wa kushiriki katika mahitaji mengine ya wanafunzi, yakiwemo sare na chakula.
Alisema wazazi wanaokataa kuchangia chakula wanapaswa kubainishwa ili suala hilo lifuatiliwe na kushughulikiwa, badala ya kuwaadhibu watoto ambao hawana uwezo wa kuamua kuhusu michango hiyo.
“Tusiendekeze haya,Wazazi wenzangu, tujifunze na kuzoea kuchangia, Kama mzazi hutaki kuchangia, unataka mtoto akale chakula cha nani?” alihoji Nyongo.
WAZAZI WALALAMIKIA MICHANGO
Agizo hilo limekuja wakati baadhi ya wazazi katika eneo hilo wakilalamikia wingi wa michango ya shule, wakisema hali hiyo inawaongezea mzigo wa gharama za elimu, hasa kwa familia zenye kipato cha chini.
Mmoja wa wakazi wa Msata, Daniel Mkali, alisema wazazi wamekuwa wakikabiliwa na michango mbalimbali inayohusisha ulinzi, mitihani, chakula, majaribio na masomo ya ziada, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kumudu gharama hizo.
Alisema wakati mwingine wazazi hutakiwa kuchangia kiasi tofauti kwa mahitaji mbalimbali, huku gharama za masomo ya ziada kwa wiki zikifikia Sh6,000, jambo alilodai kuwa ni gumu kwa familia zenye kipato kidogo.
“Unakuta mtoto anarudishwa shule. Sasa kosa lake ni nini? Kama kuwajibishwa niwajibishwe mzazi kwa ujinga wangu,” alisema Mkali.
DC NDEMANGA AWAOMBA WAZAZI KUSHIRIKIANA NA WALIMU
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, aliwataka wazazi kushirikiana na walimu kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza shuleni, ikiwemo suala la michango.
Ndemanga alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakipuuza michango ya shule, huku akibainisha kuwa katika shughuli nyingine za kijamii, ikiwemo sherehe ,mahafali, baadhi yao hushiriki kuchangia fedha.
Alitoa rai kwa wazazi kutumia mikutano ya shule kujadili na kukubaliana kuhusu mahitaji ya wanafunzi ili kuepusha migogoro na kuhakikisha watoto wanaendelea na masomo bila vikwazo visivyo vya lazima.
WANANCHI WATAJA KERO ZA BARABARA NA MAJI
Katika mkutano huo, wakazi wa Msata, akiwemo Chocha Chocha na Yusuph Ramadhani, waliwasilisha malalamiko kuhusu changamoto za barabara na upatikanaji wa maji, wakiiomba Serikali kuzifanyia kazi.
Nyongo alisema dhamira ya ziara zake ni kuwafikia wananchi katika maeneo yao, kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo na kushirikiana na viongozi pamoja na mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa kero hizo.

.jpeg)
0 Comments