
DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetwaa tuzo nne katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), zikitambua mchango wake katika kuboresha mawasiliano kwa umma, kampeni za uelimishaji na usimamizi wa mawasiliano wakati wa changamoto.
Tuzo hizo zilitolewa Oktoba 8, 2026, ambapo Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle, alisema mafanikio hayo ni chachu ya kuendelea kubuni njia bora za kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, Gowelle alisema shirika litaendelea kutumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuboresha mawasiliano na kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu huduma za umeme.
Alishukuru PRST kwa kutambua mchango wa shirika hilo, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kutoka Wizara ya Nishati, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TANESCO.
Pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika sekta ya umeme, ikiwamo kuimarisha miundombinu na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Savera Kazaura, aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, aliipongeza TANESCO kwa hatua ilizopiga katika kuboresha utoaji wa taarifa kwa wananchi, hasa wakati wa changamoto za huduma ya umeme.
Kazaura alisema taasisi za umma zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mawasiliano ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na jamii.
Alisema juhudi za TANESCO kutoa taarifa kuhusu changamoto za umeme zinapojitokeza zinapaswa kuendelezwa ili kuongeza imani ya wananchi na kuboresha huduma.

Katika tuzo hizo, TANESCO ilipata Tuzo ya Ubora katika Usimamizi wa Mawasiliano Wakati wa Migogoro (Crisis Communication Management), Tuzo ya Ubora katika Kampeni ya Elimu kwa Umma (Public Awareness Campaign) kupitia kampeni ya Nishati Safi ya Pika kwa Umeme, na Tuzo ya Idara Bora ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma (Best Public Relations Department).
Tuzo ya nne ilikwenda kwa Gowelle, aliyetangazwa kuwa Mtaalamu Bora wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Tanzania kwa mwaka 2026 (Best PR Practitioner 2026).
Tuzo za PRST hutolewa kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango wa mawasiliano katika kuimarisha sekta mbalimbali na kuongeza tija kwa wataalamu wa mawasiliano nchini.
0 Comments