Mamlaka za Urusi zimemkamata mwandishi wa habari wa Japan, Yuki Imai, kwa tuhuma za ujasusi, zikidai kuwa alikusanya taarifa zinazohusu uwezo wa ulinzi wa Moscow kwa niaba ya Tokyo.

Imai, ambaye anafanya kazi katika gazeti la Hokkaido Shimbun, alikamatwa katika eneo la Sakhalin, mashariki mwa Urusi, siku moja kabla ya ratiba yake ya kuondoka nchini humo. Baadaye alisafirishwa kwa ndege hadi Moscow, ambako mahakama iliamuru azuiliwe rumande akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake.

Serikali ya Japan imesema inatafuta maelezo zaidi kuhusu tukio hilo na haijaweza kuwasiliana na mwandishi huyo tangu alipokamatwa.

Kukamatwa kwake kunajiri wakati uhusiano kati ya Urusi na Japan ukiendelea kuzorota, hasa baada ya Rais Vladimir Putin kutembelea Visiwa vya Kuril vinavyogombaniwa na mataifa hayo mawili mwezi Agosti.

Kwa mujibu wa mamlaka za Urusi, Imai alidaiwa kufanya kazi kwa maelekezo ya idara ya ujasusi ya Japan na kukusanya taarifa kuhusu watu wanaohusika katika kile Moscow inachokiita "operesheni maalum ya kijeshi" katika Visiwa vya Kuril.

Visiwa vya Kuril viko kati ya kisiwa cha Hokkaido nchini Japan na Rasi ya Kamchatka nchini Urusi. Ingawa vinasimamiwa na Urusi, Japan inadai umiliki wa visiwa vinne vya kusini mwa eneo hilo, ambavyo inayataja kama "Maeneo ya Kaskazini".

Shirika la usalama la Urusi (FSB) lilichapisha video inayowaonyesha maafisa waliovalia barakoa wakimkamata mtu katika chumba cha hoteli kabla ya kumsafirisha hadi Moscow. Video hiyo baadaye ilimuonyesha akiwa ndani ya kizimba mahakamani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Interfax, Imai ataendelea kuzuiliwa hadi Desemba 12 kabla ya kuanza kwa kesi yake. Serikali ya Japan haijatoa tamko la kina kuhusu tuhuma zinazomkabili mwandishi huyo.