Shirika la habari la Saba, linalohusishwa na vuguvugu la Houthi nchini Yemen, limeripoti kuwa kundi hilo limetoa onyo kwa mashirika ya ndege kwamba anga ya Saudi Arabia si salama kwa safari za ndege za kiraia.

Onyo hilo linasema kuwa anga ya Saudi Arabia "itakuwa uwanja wa operesheni kwa vikosi vyetu vya kijeshi."

Onyo hilo la Wahouthi limekuja baada ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kutangaza kuwa umejiunga na mashambulizi ya kujibu mapigo yaliyoanzishwa na serikali rasmi ya Yemen dhidi ya Wahouthi.

Awali tuliripoti kuwa vikosi vya serikali ya Yemen vinasema vimeanzisha mashambulizi dhidi ya mji mkuu, kwa lengo la kuutwaa tena mji wa Sanaa kutoka mikononi mwa Wahouthi.

Kufuatia kusonga mbele kwa Wahouthi hivi karibuni ambao ni washirika wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikosi vya serikali ya Yemen vilitangaza vita dhidi yao jana.

Vikosi hivyo, ambavyo vinaungwa mkono na Saudi Arabia, vinasema pia vimechukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Mlango bahari wa Bab al-Mandab kutoka mikononi mwa Wahouthi