
DAR ES SALAAM: WALIMU nchini wametakiwa kutambuliwa na kupongezwa kwa mchango wao katika malezi na utoaji wa elimu kwa watoto, huku wakihimizwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Eugenia Kafanabo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani yaliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL).
Dk. Kafanabo alisema jamii inapaswa kuungana kuwapongeza walimu kwa kazi kubwa na ngumu wanayoifanya katika kuwafundisha na kuwalea wanafunzi.

Alisema walimu wana jukumu muhimu katika malezi ya watoto kwa kuwa, pamoja na kufundisha, wanashiriki kuwajenga kitabia na kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na maisha ya baadaye, huku wakisaidia kutekeleza jukumu la wazazi.
Mhadhiri huyo alisema wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Walimu Duniani, ni muhimu jamii kuthamini juhudi za walimu na kuwapongeza kwa kazi wanayoifanya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na malezi yanayowawezesha kukabiliana na changamoto za maisha.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma, Fausta Akaro, aliwataka walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani humo kuendana na mabadiliko ya utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA katika kutekeleza majukumu yao.

Akaro alisema matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kurahisisha shughuli mbalimbali za ufundishaji na usimamizi wa elimu, ikiwemo maandalizi ya masomo, ukusanyaji na uwasilishaji wa taarifa pamoja na takwimu za shughuli zinazotekelezwa shuleni.
Alisema walimu wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na teknolojia kuboresha ufanisi wa kazi zao na kuendana na mabadiliko yanayotokea katika sekta ya elimu.
0 Comments