DAR ES SALAAM: Kisukari cha mimba kinaweza kusababisha madhara makubwa kwa mama na mtoto iwapo hakitagundulika na kudhibitiwa mapema, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Amani Idris Kikula, amesema.

Kikula amesema hali hiyo hutokea pale mwili wa mama mjamzito unaposhindwa kutumia na kudhibiti kiwango cha sukari ipasavyo, hali inayohusishwa na kuongezeka kwa mahitaji ya insulin wakati wa ujauzito.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa afya, amesema wakati wa ujauzito mwili wa mama huhitaji kuzalisha insulin kwa kiwango kikubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya mwili na ukuaji wa mtoto.

Amesema changamoto katika kongosho au viashiria vya awali vya kisukari vinaweza kusababisha kiwango cha sukari katika damu kuongezeka.

Kwa mujibu wa Kikula, kisukari cha mimba mara nyingi huonekana kuanzia wiki ya 24 ya ujauzito, ingawa kwa baadhi ya wanawake waliokuwa na kisukari kabla ya ujauzito, hali hiyo inaweza kugundulika mapema zaidi.

Amesema kiwango cha sukari kikibaki juu bila kudhibitiwa kinaweza kuathiri ukuaji wa mtoto na kuongeza hatari ya mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mkubwa, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Kikula ameongeza kuwa kisukari kisichodhibitiwa wakati wa ujauzito kinaweza pia kuongeza hatari ya matatizo kwa mama, yakiwemo shinikizo la damu wakati wa ujauzito, kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua na maambukizi.

Kwa upande wa mtoto, amesema madhara yanaweza kuendelea hata baada ya kuzaliwa, kwani watoto wanaozaliwa kutokana na ujauzito wenye kisukari kisichodhibitiwa wanaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata uzito kupita kiasi na magonjwa yasiyoambukiza baadaye katika maisha.

Hata hivyo, Kikula amesema kugundua kisukari cha mimba mapema kunatoa fursa ya kukidhibiti na kupunguza madhara kwa mama na mtoto.

Amesisitiza umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki na kufanyiwa vipimo vinavyohitajika, akisema hatua za awali za kudhibiti hali hiyo ni pamoja na kubadili mfumo wa chakula na kufanya mazoezi yanayofaa kwa mama mjamzito.

Amesema tiba nyingine zinaweza kutolewa kulingana na hali ya mgonjwa na ushauri wa wataalamu wa afya.

Ameongeza kuwa uchunguzi wa mapema na ufuatiliaji wa karibu wakati wa ujauzito ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto na kupunguza uwezekano wa madhara wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya mtoto kuzaliwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt Irene Isaka, amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakisubiri kupata matatizo ya kiafya ndipo wanapoona umuhimu wa kukata bima ya afya.

Amesema wananchi wanapaswa kuwa na bima ya afya mapema ili waweze kupata huduma wanapohitaji badala ya kusubiri gharama za matibabu kuwa kubwa.