
BUKOBA: Wataalamu na watafiti wa zao la migomba kutoka nchi tisa barani Afrika wamefanya ziara nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika utafiti na uzalishaji wa zao la ndizi.
Ziara hiyo imefanyika katika mikoa ya Arusha na Kagera, ambapo wataalamu hao wametembelea mashamba ya wakulima na kujionea namna wanavyotumia aina mpya za migomba iliyofanyiwa utafiti, ikiwemo Fia na Taribani 1-14, ambazo zimeonesha uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwemo magonjwa, wadudu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wataalamu hao ni sehemu ya Mtandao wa Utafiti wa Zao la Migomba (BBN), unaowakutanisha watafiti kutoka Tanzania, Comoro, Nigeria, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na Ghana.

Mratibu wa Zao la Migomba, ambaye pia ni Meneja wa Utafiti wa Mazao na Utunzaji wa Mazao baada ya Mavuno kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), amesema mtandao huo ulianza shughuli zake mwaka 2024 kwa lengo la kuimarisha utafiti na upatikanaji wa mbegu bora za migomba zinazoweza kuendana na mazingira mbalimbali.
Amesema ushirikiano huo pia unalenga kusaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine zinazopunguza uzalishaji wa zao la ndizi.

Katika ziara hiyo, wataalamu hao walifanya vikao vya pamoja, kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuendeleza tafiti zinazolenga kupata aina za migomba zenye tija zaidi kwa wakulima na wazalishaji wa ndizi barani Afrika.
“Tumekuja pamoja kujadili namna ya kuimarisha utafiti wa migomba, lakini pia kuona kwa vitendo namna wakulima walivyopokea aina za migomba zinazofanyiwa utafiti. Mfano Fia imefanya vizuri, lakini pia Taribani 1-14, jamii ya matoke kwa Tanzania na Uganda, nazo zimeleta matokeo chanya,” alisema Shimwela.
Alisema kupitia tafiti zinazofanywa na taasisi za utafiti wa kilimo barani Afrika, ikiwemo TARI, jitihada zinaendelea za kupata na kusambaza aina za migomba zinazoweza kutoa uzalishaji unaoendana na mazingira ya mkulima pamoja na changamoto zinazolikabili zao hilo.

Alisema nchi nyingine wanachama wa mtandao huo zimeahidi kuendelea kuimarisha elimu kwa wananchi ili kuwawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko katika uzalishaji wa migomba na kutumia aina zilizofanyiwa utafiti.
Mbali na vikao vya wataalamu, timu hiyo ilitembelea mashamba ya wakulima katika maeneo mbalimbali na kuzungumza nao kuhusu uzoefu wao baada ya kuanza kutumia aina mpya za migomba zilizofanyiwa utafiti.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, hatua hiyo ni muhimu katika kupata mrejesho kutoka kwa wakulima, ambao ndio watumiaji wakuu wa teknolojia na aina mpya za migomba zinazozalishwa kupitia tafiti.
Miongoni mwa wakulima waliotoa uzoefu wao ni Nasoro Mpendekaki wa Kemondo, Halmashauri ya Bukoba, ambaye alisema alikumbana na changamoto ya kuachana na migomba ya asili baada ya uzalishaji kupungua na mimea kuathiriwa na ugonjwa wa Mnyauko.
Mpendekaki alisema hakukuwa rahisi mwanzoni, hasa kutokana na mtazamo wa jamii iliyomzunguka, lakini baada ya kutumia aina mpya ya Fia ameanza kuona matokeo chanya.
Alisema kwa sasa huuza mikungu kati ya 100 na 120 kwa mwezi, huku kila mkungu ukiuzwa kati ya Sh15,000 na Sh20,000, hali inayomuwezesha kupata chakula na kuboresha kipato cha familia.

“Kilimo hiki nimekirithisha pia kwa watoto wangu ambao sasa wana mashamba yao. Pia nimefungua tawi la mauzo katika Mkoa wa Tabora na nimeboresha kipato changu mara dufu kutokana na mauzo ya ndizi,” alisema.
Kwa upande wao, wajumbe kutoka nchi nyingine, akiwemo Dorcas Ibitoye kutoka Nigeria, Jean Prosper kutoka Comoro na Michael Batee kutoka Uganda, walisema ziara hiyo imewakutanisha watafiti kutoka nchi tisa zinazozalisha ndizi barani Afrika.
Walisema jambo kubwa lililojadiliwa ni namna ya kuhakikisha matokeo ya tafiti yanaondoka maabara na kuwafikia moja kwa moja wakulima, ili aina mpya za migomba ziendane na mazingira halisi ya uzalishaji.
Walisema ushirikiano huo unalenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha kipato cha wakulima na kuhakikisha tafiti za migomba zinazofanywa barani Afrika zinatoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wazalishaji wa zao hilo.
0 Comments