
Wizara ya Viwanda na Biashara imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi zake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, katika kikao kilichofanyika Bungeni, jijini Dodoma. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo (Mb), amemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara katika kikao hicho kilichohusisha Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO).
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Londo amesema Serikali, kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara ni sehemu muhimu ya juhudi za kuimarisha uzalishaji, kuwawezesha wafanyabiashara na kupanua fursa za masoko.
Kwa upande wa TanTrade, Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Balozi Mafuru, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 hadi 2025/2026. Taarifa hiyo imeainisha hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza biashara kupitia utoaji wa taarifa za masoko, uratibu wa maonesho na majukwaa ya biashara, pamoja na mafunzo na ushauri kwa wafanyabiashara.
Katika kipindi hicho, TanTrade imekusanya mapato ya shilingi bilioni 36.96, huku kampuni 12,337 zikishiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF). Aidha, wafanyabiashara 7,593 wamejengewa uwezo kupitia programu 40 za mafunzo, huku majukwaa ya biashara ya kimataifa yakiwezesha kupatikana kwa hati 24 za makubaliano zenye thamani ya shilingi bilioni 158.1.

Mafuru ameeleza kuwa mafanikio hayo yanaweka msingi wa kuendeleza utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara kupitia TanTrade kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na kuchangia kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Msisitizo umewekwa katika kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania, kuimarisha biashara ndogo na za kati pamoja na viwanda, na kupanua ushiriki wa wafanyabiashara katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Katika kuendeleza juhudi hizo, Wizara kupitia TanTrade itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine kuimarisha masoko, matumizi ya TEHAMA na uchambuzi wa taarifa za biashara. Vipaumbele vingine ni kuimarisha diplomasia ya kibiashara, kurahisisha biashara na kuboresha uwezo wa taasisi kiutendaji na kifedha ili kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wafanyabiashara na wazalishaji nchini.
0 Comments