Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema njia ipo nyeupe kwa viongozi na wanachama wanaotaka kuondoka katika chama hicho kwa sababu ya kutoridhishwa na mgawo wa viti maalum vya wanawake katika Bunge.
Akizungumza jana katika mkutano wa Baraza la Ushauri la Chadema jijini hapa, Dk. Slaa alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, yamejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanachama kwamba mikoa yao haijapata wabunge wa viti maalum licha ya kuwapo wabunge wa majimbo.
Alisema miongoni mwa mikoa inayolalamika ni pamoja na Mbeya, ambao umepata wabunge wawili wa kuchaguliwa, lakini haukupata mbunge wa viti maalum.
Watu wa Mbeya mnalalamika sana kuhusu suala la viti maalum wakati Karatu tumeibeba Chadema toka mwaka 1995 hadi sasa, lakini hatujawahi kupewa viti maalum vya ubunge. Mbeya ni juzi tu ndiyo mmeanza kuibeba Chadema, halafu mnasema mnataka kuondoka kwenye chama. Tunasema ondokeni njia nyeupe kwa anayetaka kufanya hivyo,” alisema Dk. Slaa.
Alisema viongozi wasioelewa kuhusu utaratibu wa utoaji wa viti maalum wanakuwa na ubinafsi wakati Chadema viti maalum havitolewi kama zawadi na wala siyo hisani kama wanavyodhani baadhi ya watu, bali vina malengo yake.