Serikali imefanikiwa kuipatia hospitali ya mkoa wa Shinyanga vifaa vya kisasa na kuiondolea tatizo la muda mrefu la ukosefu wa vifaa vikiwemo vya chumba cha upasuaji ambalo lilikuwa kero kubwa kwa wananchi mkoani hapa.
Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga, Mwamvua Jilumbi, alisema kuwa shehena ya mwisho ya vifaa hivyo kutoka nchini Ujerumani vimeshawasili na kupokelewa hospitalini hapo.
Baadhi ya vifaa hivyo ni mashine sita za upasuaji wa watu mahututi kwa wakati mmoja, mashine ya kieletroniki ya kufufua mtu aliyezimia na mashine ya kutambua mwenendo sahihi wa mapigo ya moyo wa mtoto awapo tumboni mwa mama yake.
Vingine ni Mashine za kisasa za kutunzia watoto waliozaliwa njiti, mashine za upasuaji wa macho, mashine za kieleroniki za kupima damu na mashine za kisasa za maabara.
Vifaa vingine ni pamoja na vitanda viwili vya kisasa vya kupasulia wagonjwa mahututi na watoto wachanga 10 na vitanda vingine vya kawaida 20.